COVID-19: Idadi jumla ya vifo vilivyothibitishwa nchini Kenya ni 1,103
Na CHARLES WASONGA
WAGONJWA wengine 10 wamethibitishwa kufariki nchini Kenya kufikia jana Jumamosi kutokana na Covid-19 na hivyo kuifanya idadi jumla ya vifo kutokana na ugonjwa huo kuwa 1,103.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Afya, watu wengine 1,065 walithibitishwa kuwa na virusi vya corona ndani ya saa 24 hadi Jumamosi hivyo kufikisha idadi jumla ya maambukizi tangu Machi 13, 2020, kuwa 61,769.
Visa hivyo vipya vilinakiliwa baada ya sampuli 7,386 kupimwa katika kipindi hicho hicho cha saa 24.
Miongoni mwa wagonjwa hao wa hivi punde, mdogo zaidi ana umri wa miaka mitatu na mzee zaidi ana umri wa miaka 104.
Kwa mara nyingine Nairobi inaongoza kwa idadi ya visa vipya vya maambukizi kwa kuandikisha visa 263 ikifuatwa na Kaunti ya Mombasa iliyoandikisha visa 181.
Uasin Gishu ina visa 63, Nakuru (62), Kisumu (47, Kajiado (38), Kilifi (36), Kericho (30), Busia (30), Baringo (26), Kakamega (25), Nyeri (21), Turkana (21), Homa Bay (20) na Trans-Nzoia imeandikisha visa 18.
Wakati huo huo, taarifa hiyo imesema kuwa jumla ya wagonjwa 888 wamepona na hivyo kufikisha idadi jumla ya waliopona corona kuwa 41,019 kufikia Jumamosi, Novemba 7, 2020.
Kati hao 824 walikuwa wakiuguzwa nyumbani ilihali 64 walipona baada ya kulazwa katika hospitali mbalimbali nchini.
Wizara hiyo inayoongoza na waziri Mutahi Kagwe ilisema kuwa wakati huu jumla ya wagonjwa 1,270 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini.
“Vile vile, wengine 5,537 wanatunzwa nyumbani wakiwa wamejitenga. Wagonjwa 56 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU), 26 wamewekewa mitambo ya kuwasaidia kupumua na wengine 27 wanaongezewa hewa ya oksijeni,” taarifa hiyo ikaeleza.
Wagonjwa wengine 80 wamelazwa katika wodi za kawaida na wengine 14 wako katika wodi ambako wanachunguzwa kwa makini (High Dependency Unit-HDU).