CECIL ODONGO: Utata wa BBI pia ulibugika miswada ya Bomas, Wako
Na CECIL ODONGO
MAKUNDI mbalimbali ya kijamii na wanasiasa wamekuwa wakijitokeza kudai kwamba, maoni yao hayakujumuishwa kwenye ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) iliyozinduliwa hivi majuzi.
Mwanachama wa jopo hilo Meja Mstaafu John Seii ndiye wa hivi punde kujitokeza kudai masuala waliyokubaliana kuhusu BBI yalibadilishwa katika ripoti ya mwisho.Eti badala yake mapendekezo ya watu “fulani” ndiyo yalijumuishwa.
Kwa mfano, alitaja suala la kuongezwa kwa maeneobunge 70 mapya kama jambo geni ambalo hawakulijadili au kuafikiana wakati wa kuoanisha mapendekezo ya mwisho.
Ingawa baadhi ya wanajopo wamekanusha madai ya Meja Seii, si siri kwa Wakenya kwamba wanachama wa jopo walikuwa watumwa wa wanasiasa.Kwanza, wanachama hao 14 walizunguka kote nchini wakitumia pesa za mlipaushuru kupokea maoni ya raia.
Japo si rahisi kuridhisha kila mtu, ingekuwa vyema iwapo masuala yanayowahusu Wakenya yangepewa kipaumbele badala ya nyadhifa za kuwatunuku wanasiasa.
Madai ya Meja Seii hayajulikani iwapo ni ya kweli au ya uongo, ila jambo lisilopingika ni kwamba wanasiasa wetu wanapigania maslahi yao kwenye ripoti hiyo.
Kando na kauli ya Bw Seii, jambo jingine ambalo limezuka ni iwapo yaliyomo kwenye ripoti yanafaa kutekelezwa jinsi ilivyo au mapendekezo zaidi yajumuishwe.
Huku chama cha ODM na mrengo wa Kieleweke zikipigia upato utekelezaji wa ripoti hiyo jinsi ilivyo, Naibu Rais na mrengo wake wa Tangatanga wanasisitizia marekebisho zaidi yafanywe kabla kura ya maamuzi.Hata hivyo, yanayokabili BBI huenda si mageni kutokana na siasa ambazo zimekuwa zikizingira mabadiliko ya Katiba nchini.
Mnamo 1990 utawala wa Kanu na upinzani ulivutana kuhusu iwapo taifa lilifaa kukumbatia mabadiliko ya Katiba, kuelekea mfumo wa vyama vingi.Mivutano hiyo ambayo ilishirikisha wanasiasa, wanaharakati wa masuala ya haki za kijamii na viongozi wa kidini, ilijaa ghasia na kusababisha mauti ya wengi.
Hata baada ya mfumo wa vyama vingi kutua nchini ilibainika kuwa suala kuu lilikuwa dondandugu la ukosefu wa uwazi katika uchaguzi mkuu.
Hali ilikuwa vivyo hivyo kwenye mabadiliko ya Katiba ya 2004/5 ambapo wataalamu walivutana kuhusu yaliyostahili kuwemo kwenye sheria kuu mpya ya nchi, wakati huo vikao vikiandaliwa katika ukumbi wa Bomas.
Itakumbukwa kuwa, mapendekezo ya Bomas yalibadilishwa hususan baada ya Yashpal Ghai kuondolewa kama Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba (CKRC), huku waliomtupa nje wakihisi uwepo wake ungeibuka na Katiba isiyowafaa.
Mwishowe, Wakenya walipopiga kura ya maamuzi mwaka 2005 walikataa mswada wa Wako ambao uliondoa baadhi ya mapendekezo kwenye mswada wa Bomas.
Vuta nikuvute hizo zilirejea wakati wa mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ya 2010 ambayo mwishowe ilipitishwa na Wakenya. Hii ni licha ya viongozi wa kidini na Naibu Rais Dkt Ruto kuipinga wakati huo.
Kwa hivyo, maoni mseto ambayo yamekuwa yakitolewa kuhusu ripoti ya BBI yanafaa kujumuishwa ili tuwe na mswada wa mawaelewano sio mvutano; na hivyo kusizuke tena juhudi zingine za kuibadilisha siku za usoni iwapo itapitishwa kwenye kura ya maoni.