• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Joho aongoza msako kusaka wanaopuuza kanuni za corona

Joho aongoza msako kusaka wanaopuuza kanuni za corona

MOHAMED AHMED Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Mombasa alishangaza wengi Jumamosi usiku wakati alipoandamana na maafisa wa polisi katika operesheni ya kukamata watu wanaokiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Bw Joho aliandamana na maafisa hao pamoja na askari wa kaunti yake katika operesheni hiyo iliyolenga sehemu inayotumiwa na wavutaji shisha.Watu 35 walikamatwa kwenye msako huo na kunasa vifaa 13 vinavyotumiwa kuvutia shisha katika eneo linalojulikana kama Escape.

Kulingana na kamanda wa polisi eneo bunge la Nyali, Bw Daniel Mumasaba, waliokamatwa walikuwa wamekiuka kanuni zote ambazo zimewekwa na serikali kupambana na corona.

“Operesheni ilikuwa kabla ya kafyu lakini ile hali waliyokuwa wamekaa ilikuwa kinyume cha sheria. Walikuwa wamesongamana, hawakuwa na barakoa na walikuwa wanavuta shisha ambayo pia ni marufuku,” akasema Bw Mumasaba.

Baadhi ya vijana walionekana wakitorokea maeneo yaliyoko karibu na bahari baada ya kugundua kulikuwa na msako.“Ni nani mwenye sehemu hii,” Bw Joho alisikika akiuliza kwenye kanda ya video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii huku polisi wakiwa wanalenga wale waliokuwa wamekaa sehemu tofauti eneo hilo.

Msako huo ulifanyika wakati Bw Joho amekuwa akihimiza wakazi kufuata kanuni zilizowekwa na serikali ili kudhibiti msambao wa corona.

Ripoti zimeonyesha kuwa Mombasa ni miongoni mwa kaunti ambazo zimekuwa zikiendelea kupata idadi kubwa zaidi ya watu wanaoambukizwa corona.

Katika mji wa Nakuru, polisi waliwakamata watu 86 katika baa moja maarufu kwenye msako waliofanya Jumamosi asubuhi.

Polisi walisema kwamba waliokamatwa walikuwa miongoni mwa wateja 500 waliokuwa kwenye klabu hicho.Kanda iliyosambazwa mtandaoni ilionyesha polisi wakirusha gesi ya kutoa machozi ndani ya klabu hiyo wateja walipowarushia chupa za pombe.

You can share this post!

Mwili wa aliyekuwa mkuu wa polisi wazikwa baada ya miaka 5

Mamlaka kuharibu bidhaa ghushi za thamani ya Sh100 milioni