• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
Corona ilitufungua macho, sasa tunavuna maelfu kwa biashara yetu

Corona ilitufungua macho, sasa tunavuna maelfu kwa biashara yetu

NA RICHARD MAOSI

Mlipuko wa janga la corona umekuja na changamoto si haba, huku idadi kubwa ya watu wanaokaa mijini,wakipoteza ajira, wengi wao wakiwa ni wafanyibiashara.

Sekta ya utalii ilisalia kuzorota, baada ya serikali kuifunga nchi kwa miezi minne. Wanafunzi wa vyuo na taasisi za kiufundi nao waliamua kurudi mashambani ama kuajiriwa kama vibarua mitaani , na kupokea malipo duni.

Lakini kwa Mary Wambui na Eunice Muthoni, pacha wa toka nitoke ambao ni wakazi wa eneo la Uthiru, Kaunti ya Nairobi, pamoja na dada yao mkubwa Ruth Wanjira, walitumia mwanya huo kufikiria jinsi ya kujikimu maishani na kujianzishia kazi ya kuuza chakula mtaani humo.

Eunice anasema walianza kazi yenyewe mnamo Machi 2020, baada ya taasisi wanayosomea kufungwa, ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kurudi nyumbani wakati wa virusi vya covid-19.

Haikuchukua muda na walipochoka kukaa nyumbani, walijadiliana kisha wakafanya utafiti wa kina wakilenga kutambua kazi ambayo ingewasaidia kujipatia kipato.

“Awali tukiwa shuleni tulikuwa na wazo la kujianzishia biashara, lakini hatukua tumeamua ni aina gani ya kazi ambayo ingefanya vyema katika eneo hili,” akasema.

Eunice na Mary wamesomea taaluma ya kuandaa vyakula katika taasisi ya PC (Paramount Chief) Kinyanjui, Nairobi.

Anasema walianzisha mradi huu kwa mtaji wa 50,000, hela ambazo zilikuwa ni akiba yao, pamoja na mchango kutoka kwa jamaa zake.

Akiba hii iliwasaidia kununua sufuria, mashine ya kupika vinanzi (chips), mashine ya kupasha joto chakula na vyombo vya kupikia na kupakulia. Aidha hela zingine zilienda kulipa kodi na kulipia umeme.

Eunice akimhudumia mteja katika mkahawa wao eneo la Uthiru, Nairobi. PICHA/ RICHARD MAOSI

Kutokana na soko la uhakika, walianza kuwauzia chakula wafanyibiashara, mafundi , waendeshaji boda na wahandisi wanaotengeneza magari katika eneo la Uthiru.

Ruth tayari alikuwa na uzoefu na tajriba katika sekta ya uuzaji chakula, na hilo lilikuwa chocheo kwa kunawiri kwa biashara hiyo licha ya ushindani kutoka kwa wawekezaji wengine.

“Nilielewa kuvutia wateja wapya kunahitaji chakula kilichoandaliwa kwa ustadi wa juu, kuwahudumia wateja kwa moyo wa kujitolea, kuimarisha usafi katika hoteli na kuhakikisha bei inalingana na mifuko yao,” Ruth aliambia Taifa Leo Dijitali.

Eunice anasema aghalabu wao huagiza chakula kutoka kaunti jirani za Nyahururu, Kiambu na Muranga, ambapo wao huandaa pilau, vibanzi,wali, viazi, chapati, chai, mahamri na lishe za kienyeji.

Kwa siku moja wanaweza kutengeneza Sh5000, ila wakati mwingine mapato hupungua hadi Sh3000 kulingana na idadi ya wateja wanaozuru mkahawa wao.

“Tukiondoa pesa za matumizi kwa siku tunaweza kutenga Sh2000 kama akiba, hesabu ambayo sio chini ya Sh6000 kwa mwezi,”alisema.

Wakazi wa mtaa huu hufurika katika mkahawa huu kwa staftahi na maankuli. PICHA/ RICHARD MAOSI

Kutokana na juhudi zao mabinti hawa wanasema, ni faida ambayo itawasaidia kupanua biashara yao siku za mbeleni na kuwaboreshea wateja huduma.

Hii ndio sababu Eunice anawaomba vijana kuiga mfano wake bila kuchagua ajira, kwa sababi kazi ni kazi muradi inaweza kukidhi mahitaji ya kila siku.

Anasema baadhi ya vijana hususan akina dada wanapenda kutumia njia ya mkato, kutafuta pesa badala ya kutumia hekima na bidii.

“Wengi wa vijana katika mtaa huu wamezoea vya bwerere, hawataki kutoa jasho. Wengi pia wamezamia katika uraibu wa dawa za kulevya na ulevi chakari. Vijana wanafaa kutumia fursa ndogo waliyo nayo kujijenga. Ni aibu kumwitisha mzazi wako hela kila mara, na alikusomesha,” anasema Mary.

Aidha anaomba serikali kuwekeza katika nguvu kazi ya vijana na kutoa mazingira mwafaka ya kufanyia biashara , mbali na kutoa mtaji wa kujianzishia biashara

Changamoto

Licha ya kutengeneza hela nzuri, Mary anasema hakuna kizuri kisichokuwa na doa maana mwezi mmoja tu baada ya kuanza biashara wezi walivunja mkahawa wao na kuiba vyombo vya zaidi ya Sh15,000.

Kutoka kushoto: Ruth Wanjira, Eunice Muthoni na Mary Wambui ambao wamewekeza kwa mkahawa kwa jina Quick Stop Cafe mtaani Uthiru, Nairobi. PICHA/ RICHARD MAOSI

Ingawa walivunjika moyo mama yao aliwatia moyo na kuwahimiza waendelee na biashara.”Hiyo ni kawaida ya biashara kwani ni lazima mtu kupata faida na wakati mwingine hasara,”alisema.

“Ni pigo ambalo lilituongezea hekima, ndiposa tukaaimarisha ulinzi kwa kuweka langoni kufuli inayofaa na kuweka camera za CCTV, kufuatilia mienendo ya watu wanaoingia na kutoka.”

Mary aliongezea kuwa chakula kinapobaki, wao hulazimika kukiuza kwa bei nafuu ama kuwapatia majirani.Hii ilikuwa ikitendeka siku za awali kabla hawajajifundisha namna ya kupima chakula.

Pia wakati mwingine wanakumbana na ushindani mkali kutoka kwa watu wanaochuuza chakula cha bei rahisi, wasiozingatia kanuni za Wizara ya Afya.

You can share this post!

Ushahidi wa Uhuru na Raila hautakikani, mahakama yaamuru

SARATANI YA MATITI: ‘Nilidhani ni ugonjwa wa wanawake...