LEONARD ONYANGO: Vijana wawe makini kabla ya kufanya uamuzi kuhusu BBI
VIJANA wanafaa kuchunguza kwa makini mswada wa Mpango wa Maridhiano (BBI) kabla ya kufanya uamuzi wa kuunga mkono au kuukataa.
Baadhi ya mambo ambayo yametiwa kwenye mswada wa BBI ili kuwavutia vijana kuunga mkono huenda yasitekelezwe baada ya kupitishwa kupitia kura ya maamuzi.
Mswada wa BBI unapendekeza kuwa vijana wanaoanzisha biashara hawatalipa ushuru kwa kipindi cha miaka saba.Kadhalika, vijana walionufaika na mikopo kutoka kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (Helb) wataanza kulipa miaka minne baada ya kukamilisha masomo yao. Muda huo unalenga kuhakikisha kuwa vijana wanapata ajira kabla ya kuanza kulipia mikopo yao ya Helb.
Chambilecho wahenga; aliyeumwa na nyoka akiona ung’ong’o hushtuka. Katiba ya 2010 imesheheni mambo tele mazuri ya kuwanufaisha vijana lakini mengi hayajatekelezwa kikamilifu.
Hivyo, hakuna hakika kwamba mambo hayo yaliyo katika mswada wa BBI yatatekelezwa.Kwa mfano, Kifungu cha 21 cha Katiba ya 2010 kinatambua vijana kuwa miongoni mwa makundi yaliyotengwa kama vile wanawake na walemavu.
Kifungu cha 55 cha Katiba kinaitaka serikali kuhakikisha kuwa vijana wanasaidiwa kupata elimu na mafunzo ya kuwapatia ujuzi.Katiba inahitaji vijana wahusishwe katika kufanya maamuzi yanayohusiana na siasa, uchumi, jamii na mambo mengineyo yanayowahusu.Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiteua wazee katika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Rais Kenyatta amewahi kunukuliwa akijitetea kuwa hateui vijana kwa sababu ni wafisadi!Katiba ya 2010 inataka vijana wasaidiwe kupata ajira na kulindwa dhidi ya kutumiwa vibaya na waajiri, wanasiasa, utamaduni hatari, na kadhalika.Mnamo 2015, Bunge lilipitisha Sheria ya Ajira ambayo ilibuni Mamlaka ya Kusimamia Ajira (NEA).
Mamlaka hiyo imetwikwa jukumu la kusaidia vijana kupata ajira. Lakini kufikia sasa hakuna ushahidi kwamba NEA imemsaidia yeyote kupata ajira.
Sheria kuhusu Kandarasi ya 2015 inahitaji asilimia 30 ya kandarasi za umma zitengewe vijana, wanawake na walemavu.Mabwanyenye wamekuwa wakishutumiwa kwa kunyakua nafasi hizo za vijana.
Matajiri wamekuwa wakisajili kampuni zao kwa kutumia majina ya vijana na kisha kunufaika na kandarasi hizi.Kadhalika, masharti makali yaliyowekwa kupata kandarasi hizi yamekuwa kikwazo kwa vijana kupata kandarasi hizi.Shirika la Takwimu nchini (KNBS) linaonyesha kuwa vijana, wanawake na walemavu walinufaika na kandarasi za Sh Sh32.74 bilioni kati ya Sh64.39 bilioni walizotengewa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2019/2020.
Masharti makali yanazuia vijana, wanawake na walemavu kunufaika na kandarasi hizo.Hivyo, vijana wanafaa kuwa makini kabla ya kuunga mkono BBI.