Siasa

Ole Lenku aidhinishwa kuwa msemaji wa jamii ya Wamaasai

November 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na Stanley Ngotho

BUNGE la Kaunti ya Kajiado, limeidhinisha kutawazwa kwa Gavana Joseph Ole Lenku kama Msemaji wa jamii ya Maasai, nafasi ambayo ilishikiliwa na marehemu William Ole Ntimama kwa muda mrefu kabla ya kifo chake miaka mitatu iliyopita.

Spika wa bunge hilo Johnson Osoi, Kiongozi wa wengi Daniel Naikuni na zaidi ya madiwani 30, jana walionyesha imani yao kwamba Gavana Lenku ataongoza jamii hiyo vyema baada ya kutawazwa na Baraza la wazee Wamaasai wiki jana.

Viongozi hao walisifu kutawazwa huko kwa Bw Lenku wakisema hatua hiyo inajiri kwa wakati hasa baada ya nyufa kuanza kuonekana katika jamii tangu kifo cha Bw Ntimama mnamo Septemba 1 2016.

Kando na madiwani hao, aliyekuwa seneta Peter Mositet, spika wa zamani wa Bunge la Nairobi Alex Ole Magelo na mwanasiasa Joseph Simel waliunga mkono kutawazwa kwa Bw Ole Lenku na kusema anatosha kujaza pengo la marehemu Bw Ntimama.