• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 3:34 PM
Wamiliki wa mikahawa walia kuponzwa na corona

Wamiliki wa mikahawa walia kuponzwa na corona

Na SAMMY WAWERU

Huku Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuhutubia taifa mnamo Alhamisi katika majengo ya bunge, wamiliki wa hoteli wanamsihi kuangazia masaibu yanayozingira sekta hiyo.

Wanalalamikia biashara yao kuendelea kuhangaishwa na makali ya ugonjwa wa Covid-19, wakitakiwa kuhakikisha wametii sheria na mikakati iliyowekwa kuzuia msambao.

Chini ya muda wa majuma kadhaa yaliyopita, visa vya maambukizi ya Homa ya corona vimeonekana kuongezeka mara dufu na kwa kasi, hasa tangu Rais Kenyatta atangaze kulegeza kanuni.

Kufuatia mkurupuko wa awamu ya pili ya corona, Wizara ya Afya ikisisitiza haja ya kuzingatia sheria na mikakati iliyopendekezwa, wamiliki wa mikahawa na hoteli wanasema idadi ya wateja imepungua kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na idadi ya juu ya wagonjwa wanaoandikishwa kila siku, wamiliki wa hoteli eneo la Zimmerman tuliozungumza nao wanasema kiwango cha wateja kimeanza kushuk,a hali inayochangia kuathirika kwa biashara zao.

“Kwa muda wa wiki mbili mfululizo, kiwango cha wateja kimekuwa kikishuka. Kwa sasa idadi ya tunaohudumia ni chini ya nusu ya tuliokuwa tukipokea Rais alipotangaza kulegeza sheria kuzuia kuenea kwa corona,” akalalamika mmiliki wa Corner Cafe.

Kwenye hotuba yake kwa taifa juma lililopita, Rais alitathmini saa za kufungwa kwa mikahawa, hoteli na vituo vya kuchuuza vyakula, na pia mabaa akitaka maeneo hayo kufungwa saa tatu jioni.

“Tunamuomba baada ya kutangaza kukaza kamba sheria alizolegeza angalau atengee sekta ya hoteli mgao wa fedha kuikwamua kwa sababu wengi wetu tunaelekea kufunga mikahawa,” akasihi mmiliki wa Planet Classic Hotel.

Wamiliki na wahudumu tuliozungumza nao wanasema ongezeko la visa vinavyoandikishwa kila siku, limesababisha wateja kupunguza ari ya kutafuta huduma za mikahawa.

Ombi la wamiliki hao kwa Rais Kenyatta linajiri wakati ambapo serikali inafanya msako mkali katika hoteli, mikahawa, mabaa na maeneo ya burudani yanayokiuka sheria na mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti msambao wa corona.

You can share this post!

BBI: Wanasiasa wang’ang’ania vinono

Afueni kwa wakulima wa Laikipia mradi wa uchimbaji wa...