Makala

Ubunifu wa mitego maalum unavyomsaidia kurina asali

November 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

Ikiwa kuna mfumo wa kiteknolojia anaopigia upatu baada ya kuukumbatia mnamo 2017, ni matumizi ya mitego ya kipekee kuteka na kunasa wadudu waharibifu katika kilimo cha matunda.

John Ndung’u ni mkulima hodari wa maembe dodo Maragua, Kaunti ya Murang’a, na ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika uzalishaji wa matunda hayo.

Anasema ikiwa kuna gharama iliyomlemea na nusra ikatize ndoto zake kuzima kiu cha maembe nchini, iite ununuzi wa dawa zenye kemikali kukabili wadudu.

Isitoshe, ni dawa zilizochakachua uhalisia wa matunda anayolima na kuyafanya kuwa hatari kwa walaji, hatua iliyoathiri soko la matunda yake.

Hata hivyo, mahangaiko hayo hatimaye yalipata ‘dawa’. Suluhu ikawa matumizi ya mitego maalum kuteka na kunasa nzi wa matunda na wadudu wengine hatari.

Kwa kawaida, nyuki huvutiwa na harufu ya kunukia na juisi ya maua, na dalili ya maembe kuanza kutunda ni kuchana maua. Sawa na miti mingine inayochana maua, kipindi cha miembe kuyachana, hualika mamia, mamia ya maelfu ya nyuki, iwapo si mamilioni.

Ni wadudu wenye manufaa na tija chungu nzima na ambao wakati alikuwa akitumia dawa zenye kemikali kuua wadudu waharibifu kwa maembe, nyuki pia walikuwa wakiangamia.

Mfumo wa mitego ya kipekee, inayotiwa dawa na molasi kukabili nzi wa matunda, Ndung’u anasema umemuwezesha kufuga nyuki, na kujipa pato la ziada kupitia uvunaji wa asali.

“Nyuki hawaharibu matunda. Baada ya kufyonza juisi kwenye maua, huenda zao. Nimeweka mizinga kadhaa katika shamba langu kuwafuga na hurina asali,” anaeleza mkulima huyo.

Kwa mwaka, wafugaji wa nyuki hurina asali mara mbili au tatu, kulingana na hali ya anga na mimea inayotegemewa kuchana maua.

Hali mbaya ya anga, magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea huathiri ratiba ya kurina asali. “Kuwepo kwa wadudu, wakulima ambao hawajakumbatia mfumo wa kilimohai kuwakabili, matumizi ya dawa zenye kemikali huua nyuki shughuli za kupulizia mimea zinapotekelezwa,” Ndung’u anaonya, akisifia matumizi ya mitego maalum anayotumia.

Nyuki ni wadudu wanaopigiwa upatu kusaidia katika uchavushaji mtambuka wa mbegu za kiume kwenye miti ya matunda, ili kufanikisha ujamiishaji.

Kati ya jumla ya miti 180 ya maembe ambayo Ndung’u amepanda kwenye shamba lake, mitatu ni ya kiume. “Nyuki wanaosaidia kusambaza mbegu wa kiume, ndio haohao wananipa asali. Mbali na mapato ya matunda, hujipa pato la ziada kupitia uuzaji wa asali,” mkulima huyo anasema, akihimiza wakulima wengine wa matunda kukumbatia matumizi ya mitego maalum kukabili wadudu na kuokoa nyuki.

Mitego hiyo iliyotengenezwa kwa mikebe ya plastiki na kwa ubunifu wa aina yake, ndani huwekwa dawa na molasi kuvutia wadudu.

Ni mfumo wa kilimohai unaosaidia kuondoa gharama ya ununuzi wa dawa kuangamiza wadudu katika matunda, hasa maembe.

Katika mchakato huo, pia unasaidia kuafikia kuwepo kwa chakula salama kiafya, yaani mazao ambayo hayajakuzwa kwa kutumia dawa zenye kemikali.

Aidha, mazao ya kilimo yaliyokuzwa kwa kutumia dawa ya wadudu na magonjwa na fatalaiza yenye kemikali, yanatajwa kuchangia kuenea kwa magonjwa hatari kama vile Saratani.

Huku akiridhia matumizi ya mitego maalum kukabili wadudu kwenye maembe, hata ingawa hakufichua kiwango cha mapato kupitia ufugaji nyuki, Ndung’u alisema asali humletea mapato mazuri.