Habari Mseto

Boga na Mwashetani washtakiwe kwa wizi wa mahindi – EACC

November 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MAAFISA wakuu katika Wizara ya Kilimo wakiongozwa na Katibu Hamadi Boga na Mbunge wa Lungalunga Khatib Mwashetani wanakabiliwa na hatari ya kushtakiwa kwa sakata ya uagizaji wa mahindi ya thamani ya Sh1.8 bilioni mnamo 2017.

Katika ripoti iliwasilishwa bungeni Jumanne, Novemba 10, 2020, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inapendekeza kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji awafunguliwe mashtaka kwa makosa mbalimbali ya ufisadi.

EACC inasema kuwa uchunguzi wake umebaini kuwa Bw Mwashetani ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Blackstone ambayo ililipwa Sh792.5 milioni licha ya kwamba kampuni hiyo haikuwa imepewa zabuni.

“Uchunguzi pia ulionyesha kuwa kampuni ya Blackstone Investment haikuwa imealikwa kuwasilisha ombi la zabuni. Lakini ilipewa kandarasi ya kuwasilisha mahindi kinyume na Sheria ya Ununizi na Uuzaji wa Bidhaa za Umma (PPDA),” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak kwenye ripote ya pili ya utendakazi wake kati ya miezi ya Aprili 1, 2020 na Juni 2020.

“Uchunguzi pia ulibaini kuwa mbunge huyo ana uhusiano na kampuni ya Blackstone Investment Ltd na alifaidi kutokana na fedha zilizolipwa kampuni hiyo,” ripoti hiyo inaongeza.

Profesa Boga na maafisa wengine wa wizara ya kilimo walipatikana na hatia kutoa Sh1.8 bilioni kutoka kwa akaunti za Hazina ya Shirika la Uhifadhi wa Kimkakati wa Chakula (SFR) katika Benki Kuu kwa ajili ya kuingiza mahindi nchini Kenya mnamo 2018.

EACC iligundua kuwa maafisa hao walitoa pesa hizo bila idhibi ya Bodi ya SFR, hatua ambayo ni kinyume na Kanuni za Sheria ya Usimamizi wa Pesa za Umma (PFM Act).

Pesa hizo zilitolewa mwaka jana Wizara ya Kilimo na kulipwa kampuni ya kibinafsi kama malimbikizi deni kwa mahindi yaliyonunuliwa katika mwaka wa kifedha wa 2016-2017.

Ununuzi huo ulifanyika wakati ambapo Willy Bett ndiye alikuwa Waziri wa Kilimo lakini malipo yalitolewa wakati ambapo Bw Mwangi Kiunjuri ndiye alikuwa Waziri.

Bw Kiunjuri ni miongoni mwa maafisa wakuu wa Wizara ya Kilimo waliohojiwa na wapelelezi wa EACC kuhusiana na sakata hiyo.

Waziri huyo wa zamani pia alihojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu wa Fedha za Umma (PAC) iliyochunguza sakata hiyo. Hata hivyo, ripoti ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Ugunja haikupendekeza kushtakiwa kwa Kiunjuri.