Corona: Washukiwa wahepa mahakama

Na WAANDISHI WETU

POLISI wanakumbwa na changamoto jipya katika vita dhidi ya virusi vya corona, kwani washukiwa wanaowakamata kwa kukiuka kanuni za kupambana na janga hilo wanatoweka.

Tangu wikendi, polisi wamekuwa wakiendeleza msako ambapo watu wanaopatikana wakikiuka kanuni za kupambana na Covid-19 huachiliwa kwa dhamana, na kuhitajika kujiwasilisha mahakamani baadaye.Mnamo Jumatatu, polisi walilazimika kuomba mahakama itoe agizo la kukamatwa kwa washukiwa 16 ambao hawakufika mahakamani Nakuru.

Walikuwa miongoni mwa 131 ambao walinyakwa wikendi.Hakimu Mwandamizi Mkuu, Bi Lilian Arika alikubali ombi hilo.Katika eneo la Pwani, zaidi ya vilabu 10 vimefungwa kwa kutozingatia masharti yaliyowekwa.

Mshirikishi wa usalama katika eneo la hilo Bw John Elungata alisema kuwa zaidi ya watu 500 pia wamekamatwa kwa kuvunja sheria tangu Novemba 4.

Katika Kaunti ya Kiambu, watu wapatao 38 kutoka Thika walishtakiwa katika mahakama ya Thika kwa kukosa kuvalia barakoa.Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya hakimu mkuu Bw Oscar Wanyaga, ambaye alitoa onyo kwa yeyote atakayeletwa mahakamani kwa mara nyingine akisema atapata adhabu kali.

Shtaka lilieleza kuwa mnamo Novemba 9, 2020, katika maeneo tofauti kama Thika mjini, Juja, na Witeithie, washtakiwa walipatikana wakitembea bila kuvalia barakoa.

Walitozwa faini ya Sh5,000 kila mmoja ama kifungo cha wiki tatu gerezani.Kwingineko, Uasin Gishu, karibu watu 50 walishtakiwa Jumatatu katika mahakama ya Eldoret kwa kukaidi kanuni za Covid-19.

Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Turbo Edward Masibo, alisema washtakiwa walikamatwa na maafisa wa polisi wakati wa msako mpya uliofanywa katikati mwa mji huo na viungani mwake.

Walishtakiwa kwa makosa tofautitofauti ikiwa ni pamoja na kuuza vileo bila kuzingatia sheria za afya kuhusu maambukizi ya virusi vya corona.Wote walikiri mashtaka hayo.

Korti iliwatoza faini ya kati ya Sh500 na Sh10,000 kulingana na kosa ya kila mshtakiwa.Katika Kaunti ya Kilifi, jumla ya shule nne za upili katika maeneo ya Malindi na Magarini kaunti ya Kilifi, zimethibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya corona kufikia sasa.

Katibu mkuu wa chama cha walimu KNUT katika maeneo hayo mawili Fredrick Nguma, alisema shule hizo ni pamoja na shule ya upili ya Marafa, Majenjeni, Kibokoni na ile ya Muyeye.

Akizungumza na Taifa Leo Nguma alisema kwa sasa shughuli za masomo katika shule ya upili ya Marafa, zimesitishwa kwa muda kufuatia maambukizi hayo.Katibu huyo pia aliitaka wizara ya afya kuendeleza mpango wa kuwapima walimu, wanafunzi pamoja na wafanyakazi wengine ili kujua afya yao.

Ripoti za Joseph Openda, Lawrence Ongaro, Titus Ominde, Mishi Gongo na Alex Amani

Habari zinazohusiana na hii