• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
Pfizer inajuaje nitapata virusi vya corona? – Kagwe

Pfizer inajuaje nitapata virusi vya corona? – Kagwe

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya, Mutahi Kagwe ametilisha shaka ubora wa chanjo dhidi ya Covid-19 ambayo kampuni ya kutengeneza dawa, Pfizer, ilisema ina uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.

Akiongea alipokuwa akitoa maelezo kuhusu masuala mbalimbali kuhusu janga hilo mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Afya, Bw Kagwe alisema haamini uvumbuzi wa chanjo hiyo utaokoa ulimwengu dhidi ya ugonjwa huo hatari.

“Nimesikia juzi kwamba kampuni ya Pfizer imevumbua chanjo. Lakini binafsi naishuku. Wanasema chanjo hiyo inamzuia mtu kupata virusi hivyo. Kwanza, unajuaje nitapata virusi hivyo?” akauliza huku akiongeza kuwa kile ambacho anaweza kuamini ni dawa ya kutibu Covid-19 sio chanjo ya kuzuia mtu kupata virusi.

Bw Kagwe aliwaambia maseneta wanachama wa kamati hiyo, wakiongozwa na Michael Mbito (Seneta wa Trans Nzoia) kwamba, juhudi za kusaka dawa ya Covid-19 zinaweza kuchukua muda wa kati ya miaka mwili na mitatu.

Mnamo Jumatatu, kampuni ya Pfizer na nyingine ya Ujerumani kwa jina BioNTech zilisema chanjo hiyo mpya imebainika kuwa na asilimia 90 ya uwezo wa kukinga mtu dhidi ya kuambukizwa virusi vya corona.

Kampuni hizo pia zilisema, dawa hiyo haikuonyesha madhara yoyote kwa wagonjwa waliotumiwa kuifanyia majaribio.

Pfizer inatarajiwa kuanza kuwapa watu chanjo hiyo nchini Amerika, wale ambao wana umri wa kati ya miaka 16 na 85. Taifa hilo ni mojawapo ya nchi ambazo zimeathiriwa zaidi na janga hilo kwa kuandikisha zaidi ya maambukizi 10 milioni na zaidi ya vifo 238,000

Kenya ina jumla ya maambukizi 65,804 na vifo 1,180 kufikia jana.

You can share this post!

Sitaomba msamaha, Magoha awaambia wakosoaji

Makanisa yatishia kupinga BBI