• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 2:10 PM
Kocha wa APR aapa kuzima Gor Mahia

Kocha wa APR aapa kuzima Gor Mahia

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Mmoroko Mohamed Erradi Adil amejaa imani kuwa klabu ya APR itakuwa tayari kusambaratisha Gor Mahia katika mechi za Klabu Bingwa Ulaya.

Mabingwa hao wa Rwanda wanatarajiwa kualika miamba wa Kenya, Gor, mnamo Novemba 27 jijini Kigali kabla ya kuzuru Kenya kwa mechi ya marudiano mnamo Desemba 4. Michuano hiyo ni ya kufuzu kuingia raundi ya kwanza.

APR ilikutanishwa na Gor wakati Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) lilifanya droo mnamo Novemba 9 jijini Cairo, Misri.

Kwa mujibu wa gazeti la New Times nchini Rwanda, Erradi alisifu Gor Mahia kama “timu bora nchini Kenya na moja ya timu kali katika eneo la Afrika Mashariki’, lakini akasisitiza kuwa APR itakuwa tayari kwa kibarua kilicho mbele yake.

“Tunataka kufika mbali kwenye mashindano haya kwa hivyo lazima tuwe tayari kwa mechi hizo mbili dhidi ya Gor Mahia. Tutafanya kila tuwezalo kutinga katika raundi ijayo,” aliapa kocha huyo wa zamani wa Bechem United (Ghana) aliyewahi kuwa naibu wa kocha wa Raja Casablanca (Morocco) na pia mkurugenzi wa kiufundi wa Ittihad Tangier (Morocco) kabla ya kutua APR mwezi Julai 2019.

Erradi aliongeza Alhamisi, “Gor ni timu ngumu, na pengine inatuzidi kwa uzoefu kwenye Klabu Bingwa. Kibarua hakitakuwa rahisi, lakini hatutakuwa na kijisababu wala njia ya mkato. Lazima tupiganie matokeo mazuri tunayotafuta.”

APR ilinyakua tiketi ya kushiriki Klabu Bingwa baada ya kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda kwa mara ya 18.

Vijana wa Erradi hawakupoteza mchuano ligini msimu uliopita nao Gor wanaonolewa na Mbrazil Roberto Oliveira. Kupata tiketi ya Klabu Bingwa, Gor pia ilishinda Ligi Kuu ya Kenya. Gor ni mabingwa mara 19 wa Kenya.

Mshindi kati ya Gor na APR atafuzu kumenyana na mshindi kati ya CR Belouizdad (Algeria) na Al Nasr (Libya) katika raundi ya kwanza kati ya Desemba 22, 2020 na Januari 6, 2021.

Mshambuliaji matata wa zamani wa Gor Mahia, Jacques Tuyisenge ni mmoja wa wachezaji tegemeo wa APR.

You can share this post!

Ageukia kilimo cha penino baada ya matundadamu kumpiga...

Mbona mapasta huwabaka waumini?