Michezo

KRU yaita wanaraga wa Shujaa kambini

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Raga la Kenya (KRU) limewaita kambini jumla ya wanaraga 29 ambao kwa sasa watafanyiwa vipimo vya afya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 za kikosi cha wachezaji saba kila upande, Shujaa.

Mbali na kujiandaa kwa Raga ya Dunia, Shujaa inapania pia kujifua kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo itakayoandaliwa nchini Japan mnamo Julai-Agosti 2021 baada ya kuahirishwa mwaka huu kwa sabau ya corona.

Mbali na ukaguzi wa kawaida utakaolenga kubaini hali zao za afya na uwezo wa miili kuhimili mazoezi makali, wanaraga wote ambao wameitwa kambini mwa Shujaa watafanyiwa vipimo vya corona kwa mujibu wa kanuni za mpya za serikali katika juhudi za kudhibiti msambao wa virusi vya corona. Vipimo hivyo vitafanyika katika uwanja wa RFUEA, Nairobi.

Kati ya wanaraga ambao watategemewa na kocha mpya Innocent ‘Namcos’ Simiyu katika kampeni zijazo za Shujaa ni nahodha Andrew Amonde, kigogo Collins Injera anayeshikilia rekodi ya ufungaji wa idadi kubwa zaidi ya trai, Oscar Ouma, Willy Ambaka na Oscar Dennis.

Watano hao walikuwa sehemu ya kikosi cha SFX10 cha Afrika Kusini kilichonogesha kivumbi cha dunia cha wanaraga 10 kila upande cha IPL World 10’s nchini Bermuda majuzi.

Wanaraga wa Shujaa wanatazamiwa kuanza mazoezi baada ya kila mmoja wao pamoja na maafisa wote wa benchi ya kiufundi kupokea matokeo yao ya vipimo vya Covid-19.

Shirikisho la Raga Duniani (WR) tayari limefutilia mbali duru nne za kwanza za za Dubai, Cape Town, Sydney na Hamilton katika kampeni za Raga ya Dunia msimu ujao wa 2020-21. Ina maana kwamba kipute cha Raga ya Dunia katika msimu wa 2020-21 kinaweza tu kung’oa nanga mnamo Machi 2021 kwa duru za Los Angeles (Amerika) na Vancouver (Canada).

Mbali na raga ya wachezaji saba kila kwa upande wa wanaume, Kenya itawakilishwa kwenye fani mbalimbali katika Olimpiki za Tokyo, Japan  zikiwemo mbio za marathon, voliboli (wanawake), ndondi na taekwondo (wanawake na wanaume) na kupiga mbizi au uogeleaji (wanawake na wanaume).

“Nitategemea wanaraga waliopo kwa sasa katika orodha hii ya wachezaji wa Shujaa kabla ya kuwaweka kwenye mizani kwa mujibu wa viwango tunavyovihitaji. Tutaongeza orodha hiyo baadaye kwa kuleta wanaraga wapya kwa kuwa baadhi ya wachezaji tulionao kikosini wana mikataba inayoelekea kutamatika,” akasema Simiyu.

Simiyu, 37, aliteuliwa upya na Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) mwanzoni mwa Septemba 2020 kunoa timu ya taifa baada ya Paul Feeney wa New Zealand kugura mwezi Juni.

 

KIKOSI CHA SHUJAA:

Andrew Amonde, Vincent Onyala, Jacob Ojee, Geoffrey Okwach, Johnstone Olindi, Levy Amunga (KCB); Collins Injera, Billy Odhiambo, Daniel Taabu, Tony Omondi, Mike Okello (Mwamba); Sammy Oliech, Alvin Marube (Impala); Willy Ambaka, Herman Humwa, Eden Agero (Harlequins), Oscar Ouma, Nelson Oyoo (Homeboyz); Jeffrey Oluoch, Bush Mwale, Alvin Otieno (Nakuru); Harold Anduvate, Derrick Keyoga, Mark Kwemoi (Oilers); Daniel Sikuta, Brian Tanga (Kabras); Oscar Dennis, Dennis Ombachi (Nondescripts); Archadius Khwesa (Blak Blad).