Corona yafifisha utamu wa Maulidi
Na KALUME KAZUNGU
HAFLA ya kila mwaka ya Maulidi imeanza rasmi kisiwani Lamu huku ikikosa shamrashamra zake za kawaida kutokana na changamoto ya maradhi ya Covid-19.
Hali hiyo imepelekea mambo mengi muhimu ambayo huandaliwa wakati wa sherehe za Maulidi kufutiliwa mbali katika harakati za kutii masharti ya Wizara ya Afya nchini ili kuepuka kusambaa kwa virusi vya corona.
Sherehe za Maulidi huandaliwa kila mwaka na baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu ili kukumbuka kuzaliwa kwa Nabii Mtume Mohamed (S.A.W) katika mji mtakatifu wa Mecca katika mwaka wa 570AD.
Sherehe hizo huadhimishwa kila mwezi wa tatu wa mwaka katika kalenda ya Kiislamu.
Kila mwaka sherehe za Maulidi huhudhuriwa na wenyeji, wageni na watalii kati ya 15,000 na 20,000 lakini idadi hiyo inatarajiwa kupungua mwaka huu.
Mara nyingi wageni na watalii wanaohudhuria hafla hiyo hutoka nchi za Tanzania, Zanzibar, Unguja, Milki za Kiarabu, Mashariki ya Kati, Yemen, Omani, Marekani, na sehemu nyingine za ulimwengu mbali na Wakenya kutoka maeneo tofauti.
Katika mahojiano na Taifa Leo, Afisa wa Uhusiano Mwema wa Taasisi ya Riyadha mjini Lamu, ambayo ndiyo mwandalizi mkuu wa Maulidi, Bw Bahsan Aidarus, alisema wameafikia kufutilia mbali ngoma, mchezo wa kirumbizi na viambata vingine kwenye hafla ya mwaka huu ya Maulidi ili kutoa mwanya kwa wakazi kuepuka kutangamana, hivyo kujikinga dhidi ya corona.
Shughuli nyingine ambazo hazitaandaliwa ni kambi ya matibabu ya bure ambayo huandaliwa kila mwisho wa hafla ya Maulidi.
Miongoni mwa mambo yaliyoruhusiwa kuendelea ni mashindano ya mbio za punda, uogeleaji na mashindano ya kuendesha mashua na jahazi.
Alisema pia waumini wataruhusiwa kukariri mashairi na kushiriki usomaji wa Kurani na maombi msikitini japo kwa kuzingatia kanuni za Wizara ya Afya ili kuepuka msambao wa Covid-19.
Bw Aidarus aliwataka wanaohudhuria hafla ya Mauli mjini Lamu kutii sheria zote zinazoambatana na Wizara ya Afya kuhusiana na ugonjwa hatari wa Korona.
“Sherehe za mwaka huu za Maulidi zimeanza rasmi lakini zitakuwa tofauti kwani baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakiandaliwa kila wakati sherehe zinapofanyika yamefutiliwa mbali kwa sababu ya corona. Ombi letu kwa wanaohudhuria sherehe hizo ni kwamba watii kanuni zote za Wizara ya Afya kwa manufaa yetu,” akasema Bw Aidarus.
Sherehe hizo zinatarajiwa kufikia ukingoni kesho asubuhi.
Baadhi ya wakazi waliozungumza na Taifa Leo walieleza kusikitishwa kwao na jinsi Covid-19 inavyochangia kusambaratika kwa masuala mbalimbali nchini.
Bw Hassan Abdalla alisema kutokana na Covid-19, watalii ambao wangeshiriki hafla ya Maulidi na kunogesha biashara Lamu hawataweza kuwasili.
Bi Umu Ali alitaja kufutiliwa mbali kwa kambi za matibabu ya bure wakati wa Maulidi kuwa pigo kubwa kwa watu wengi Lamu.
Mara nyingi kambi hizo za matibabu ya bure hutekelezwa na madaktari na wataalamu wengine wa afya kutoka maeneo mbalimbali ya Kenya na ulimwenguni.