LUCY DAISY: Serikali ielewe uchumi umezorota, iwaruhusu wanawake fursa wachuuze bidhaa
Na LUCY DAISY
NCHINI Kenya, kuna wanawake wengi sana ambao hawana namna ya kujipatia riziki. Hawana kazi ilhali wana watoto na familia zinazowategemea. Hivyo basi wanabaki kukimbilia njia mbadala za kujipatia riziki.
Kwa mfano mjini Nairobi, kuna wanawake wengi tu wanauza nguo na chakula kandokando ya barabara. Baadhi wanachuuza huku wamebeba watoto wachanga.
Uchuuzi barabarani ni haramu, na mara kwa mara wanawake hawa hufurushwa na askari wa jiji. Cha kusikitisha ni jinsi askari hawa hutekeleza kazi yao pasina heshima wala huruma.
Wanawachapa viboko akinamama huku wengine wakiwaangusha chini kana kwamba ni vita. Isitoshe, wanamwaga bidhaa zao na kuzikanyagia chini. Unyama huo!
Majuzi nilipokuwa mjini niliwaona askari hawa wakimkamata mwanamke aliyekuwa amebeba mtoto mchanga, wakamcharaza viboko na hata kumuumiza mtoto huyo kando na kuharibu bidhaa alizokuwa akiuza mama huyo.
Mama alilia kwa uchungu akiwarai wamuonee huruma kwani asipofanya kazi ile, hana namna nyingine kabisa ya kuwalisha wanawe na hivyo watakufa njaa.
Ni kweli kwamba kulingana na sheria wachuuzi hawafai kutandika na kuuza bidhaa zao kando ya barabara za mjini.
Lakini serikali haina budi kuelewa kwamba uchumi umezorota na wengi wa wanawake hawa hawana namna nyingine yoyote ya kujipatia riziki.
Ni bora serikali itoea fedha na zile za kaunti zitenge mahali maalum ambapo wachuuzi hawa wanaweza kufanya kazi yao bila bughudha ili angalau wajipatie kibaba cha kila siku.
Wanawake hawa pia hawana budi kufuata kanuni watakapoagizwa kuchuuza bidhaa zao katika maeneo hayo maalum yakatayotengwa, badala ya kuuzia kandokando ya barabara ambapo husababisha msongamano kupindukia wa watu na hatari ya ajali kutokea.
Serikali pia iwaagize askari wake waache kuhangaisha wanawake hawa bila heshima. Wasiwachape na kuwakimbiza kikatili wakiwaumiza na kuwadunisha.
Iwapo lazima wawakamate, wafanye upole na kuwapeleka katika kituo cha polisi ili wafunguliwe mashtaka.
Wateja nao watambue ni makosa kwa yeyote kuuza bidhaa kando ya barabara na pindi wanawake hao watapewa eneo maalum la kuendesha biashara zao, waelekee huko kuendelea kununua bidhaa zao.
Wasiwe wavivu wa kusema sharti waletewe bidhaa katikati ya mji mahali walipo, eti hawataki kusumbuka kwenda mbali kuzinunua.
Uchumi wa nchi yetu umezorota na kila mtu anajaribu juu chini kutafuta riziki.Hakuna aliyechagua kuwa maskini.
Wanawake hawa kama binadamu mwingine yeyote wana haki ya kupewa nafasi ya kujitafutia riziki kwa upole. Polisi na wananchi kwa jumla hawana budi kuwaelewa na kuwaheshimu wanawake hawa.