Elijah Manangoi naye pia apigwa marufuku kwa kutumia pufya
Na GEOFFREY ANENE
ELIJAH Motonei Manangoi ni mwanamichezo wa hivi punde kuingia katika mabuku mabaya ya wakiukaji wa sheria za Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya duniani (WADA).
Bingwa huyo wa mbio za mita 1,500 wa Afrika, Jumuiya ya Madola na Dunia alivunja sheria inayojihitaji wanamichezo kusema waliko kila wakati.
Amepigwa marufuku miaka miwili mnamo Novemba 10, 2020. Marufuku hiyo inaanza kutumika kutoka Desemba 22, 2019.
Motonei,27, ambaye ni kakaye bingwa wa dunia wa chipukizi wa mbio za mita 1,500 George Manangoi, ni Mkenya wa pili maarufu wa mbio hizo za kuzunguka uwanja mara tatu kuadhibiwa kwa sheria zinazolenga kuweka safi mashindano baada ya Asbel Kiprop.
Bingwa wa zamani wa Olimpiki na Dunia Kiprop,31, yuko nje ya riadha baada ya kupatikana mwaka 2017 na kosa la kutumia dawa ya aina ya EPO iliyopigwa marufuku. Anatumikia marufuku ya miaka minne.
Motonei anaruhusiwa kukata rufaa dhidi ya adhabu hiyo kutoka kwa Kitengo cha Maadili cha Shirikisho la Riadha Duniani (AIU).
Tangu mwaka 2004, zaidi ya Wakenya 140 wamekipata upande mbaya wa sheria za WADA kwa kutumia dawa haramu, kukwepa kupimwa ama kukosa kutangaza wanakopatikana na kupigwa marufuku.
Baadhi ya majina makubwa yanayotumikia marufuku ni bingwa wa Olimpiki mbio za kilomita 42 Jemima Sumgong, mshindi wa zamani wa mbio za kifahari za Boston na Chicago Marathon Rita Jeptoo na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya mbio za wanaume ya kilomita 42 Wilson Kipsang’.
Kids cha Motonei kujipata motoni kinaongeza presha kwa Kenya ambayo mwaka 2016 nusura ifungiwe nje ya Michezo ya Olimpiki iliyofanyika mjini Rio de Janeiro nchini Brazil kwa sababu ya visa vingi vya ukiukwaji wa sheria za WADA na pia kutopatia Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya la Kenya (ADAK) nguvu za kisheria na kifedha za kukabiliana na maovu hayo.
Iliponea baada ya Bunge kupitisha sheria muhimu za kupatia ADAK nguvu. Hata hivyo, visa vinavyozidi kushihudiwa vinaiweka Kenya katika hatari ya kupigwa marufuku na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kushiriki ama kuandaa riadha za kimataifa.