• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Hakuna ithibati kura za Trump ziliibwa – Wakuu wa uchaguzi

Hakuna ithibati kura za Trump ziliibwa – Wakuu wa uchaguzi

NA AFP

MAAFISA wakuu wa uchaguzi nchini Amerika, Alhamisi walisema kwamba hakuna ushahidi kwamba kura za urais zilipotea, kubadilishwa au upigaji wa kura kuvurugwa anavyodai Rais Donald Trump na chama chake cha Republican.

Kauli ya maafisa hao inajiri siku ambayo Joe Biden aliendelea kupanua ushindi wake dhidi ya Trump kwa kutangazwa mshindi jimbo la Arizona na maseneta wa chama chake cha Democratic wakimlaumu Trump kwa kutia sumu sifa za nchi hiyo.

Maafisa hao wanaohusika na usalama wa uchaguzi kote Amerika, walikanusha madai ya Trump kwamba uchaguzi ulikumbwa na wizi wa kura, karatasi za kura zilipotea na kwamba alishinda uchaguzi huo wa wiki jana.

“Uchaguzi wa Novemba 3 ulikuwa wenye usalama zaidi katika historia ya Amerika,” maafisa hao walisema kwenye taarifa.“Hakuna ushahidi kwamba mfumo wa upigaji kura ulivurugwa kwa njia yoyote, kura kupotea au kubadilishwa,” walisema.

“Ingawa tunajua kwamba kuna madai mengi yasiyo na msingi na kupotosha kuhusu mfumo wa uchaguzi wetu, tunawahakikishia kuwa tuna imani kabisa katika usalama na uadilifu wa uchaguzi wetu na kila mmoja anafaa kuuamini,” walisema.

Taarifa hiyo ilitolewa na shirika la Election Infrastructure Government Coordinating Council na Cybersecurity and Infrastructure Security Agency (CISA) linalohakikisha usalama wa kura.

Ilitiwa sahihi na wakuu wa muungano taifa unaoshirikisha wakurugenzi wote wa uchaguzi wa majimbo na muungano wa taifa wa mawaziri wa majimbo ambao husimamia uchaguzi katika kiwango cha majimbo na mwenyekiti wa tume ya kushughulikia uchaguzi ya Amerika (Election Assistance Commission).

Taarifa hiyo ilitolewa saa chache baada ya Trump kutoa madai yasio na msingi kwamba kura zake 2.7 milioni zilifutwa kote nchini na nyingine kubadilishwa kuwa za Biden hasa katika jimbo la Pennsylvania na majimbo mengine.

Dai hilo lilikuwa miongoni mwa madai mengi feki ambayo Trump na chama chake cha Republican wamekuwa nayo ili kukataa ushindi wa Biden.

Kampuni ya Dominion Voting Systems ambayo Trump alidai ilifuta kura zake na serikali ya Pennsylvania ilikanusha madai ya Trump.Taarifa ya maafisa wa usalama wa uchaguzi pia ilijiri ripoti zikisema kwamba huenda Trump akamfuta mkuu wa CISA, Chris Krebs, ambaye amekuwa akikanusha madai yasiyo na msingi kwamba kura ziliibwa.

Licha ya hayo, uvumi na habari zilizosukwa kuonyesha kwamba Trump alipokonya ushindi zilifurika katika intaneti huku Trump na wanachama wa Republican wakiwasilisha kesi nyingi kote nchini kuhusu udaganyifu katika uchaguzi.

Kufikia sasa hawajafaulu kuthibitisha kesi hata moja.Taarifa ilisema kwamba maafisa wa uchaguzi kote nchini wanaendelea kukagua kura katika maeneo yao kabla ya kuthibitisha matokeo.

You can share this post!

Anyakwa baada ya kubaka msichana

Pigo kwa ODM kumpoteza Hatimy Mombasa