Habari Mseto

Mpango wa kuondoa matatu jijini utakamilika hivi karibuni – Badi

November 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

MPANGO wa kuondoa magari ya uchukuzi wa umma katikati ya jiji la Nairobi unakaribia kukamilika, Idara ya Huduma za jiji la Nairobi (NMS), imesema.NMS imetangaza maeneo mapya ambayo matatu zitakuwa zikishukisha na kubebea abiria.

Kwenye taarifa Ijumaa, Mkurugenzi Mkuu wa NMS, Meja Jenerali Mohammed Badi, alisema shirika lake limekuwa likishirikiana na Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama (NTSA) kufanikisha mpango huo kwa kujenga vituo vya mabasi nje ya jiji.

Alisema Mamlaka ya Barabara Kuu (KeNHA) tayari imepata ardhi ya kujenga vituo hivyo.Matatu zinazotumia barabara za Ngong, Lang’ata kutoka Kawangware, Kikuyu, Kibera, Lang’ata, Rongai na Kiserian zitakuwa zikishukisha abiria katika kituo cha Green Park ambacho kinajengwa karibu na bustani ya Uhuru Park.

Matatu zinazotumia barabara za Waiyaki, Uhuru Highway, Kipande na Limuru zitakuwa zikishukisha abiria katika kituo cha Fig Tree mtaani Ngara huku zinazotumia barabara za Mombasa kutoka mitaa ya South B, South C, Industrial Area, Imara Daima, Athi River, Kitengela na Machakos, zikitamatishia safari zao katika kituo kinachojengwa katikati ya makutano ya barabara za Bunyala Workshop.

Kituo cha matatu cha Muthurwa kitaendelea kutumiwa na matatu zinazotumia barabara za Jogoo na Lusaka.