Kimataifa

Trump atemwa na mawakili wake katika kesi ya uchaguzi

November 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MASAIBU ya Rais wa Amerika anayeondoka Donald Trump yameongezeka baada ya kutemwa na mawakili aliokodi kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika jimbo la Pennsylvania.

Kampuni ya mawakili ya Porter Wright Morris & Arthur ilitangaza Ijumaa kwamba imejiondoa katika kesi hiyo iliyowasilisha kwa niaba ya Trump.

Hatua hiyo imejiri siku moja baada ya Rais mteule Joe Biden kutangazwa mshindi katika jimbo la Arizona mnamo Alhamisi. Ushindi huo umemweka Biden kifua mbele kwa kuwa na jumla ya kura za wajumbe 290 dhidi ya 217 zake Trump.

Stakabadhi ambazo gazeti la The New York Times lilifaulu kuona, zilisema: “Walalamishi na Porter Wright wamefikia makubaliano ya pamoja kwamba itawafaa zaidi ikiwa Porter Wright itajiondoa.” Kampuni hiyo iliwasilisha kesi hiyo kwa niaba ya kundi la Trump jimboni Pennsylvania siku tatu zilizopita.

Hata hivyo, haijatoa maelezo au sababu za kujiondoa kwake ghafla kutoka kesi hiyo.Awali, mawakili wake walidai kuwa tume ya uchaguzi jimboni Pennslyvania ilikuwa na mifumo “miwili ya uchaguzi” ambapo wapiga kura wengine walipendelewa kuliko wengine.

Lakini mapema wiki iliyopita, gazeti la The Times liliripoti kuwa mivutano ya kindani ilichipuza katika kampuni ya Porter Wright Morris & Arthur kuhusiana na huduma za kisheria ambazo imekuwa ikitoa kwa Rais Trump na wanaoendesha kampeni zake.

Haijabainika ikiwa kampuni nyingine itapewa kazi ya kumpigania Trump baada ya kujiondoa kwa kampuni hii.Lakini Mkuu wa Sheria katika jimbo la Pennsylvania Josh Shapiro alipuuzilia mbali kesi ya rais huyo akisema haina “mashiko”.

Badala yake alishikilia kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulisimamiwa na wawakilishi wa vyama vya Democrat na Republican na “iliendeshwa kisheria, kwa njia huru na yenye kuzingatia haki.”

Kura 20 za wajumbe wa Pennsylvania ndizo zilithibitisha ushindi wa Biden Jumamosi wiki iliyopita na kuzika matumaini ya Trump kuongoza kwa muhula wa pili.Tangu wakati huo Trump amekuwa akitoa madai kadhaa kwamba kura zake ziliibwa na kuapa kuwasilisha kesi kortini kupinga matokeo ya majimbo mbalimbali.

Alidai kuwa mji mkubwa wa Pennsylvania, Philadelphia, una mfumo wa uchaguzi “uliooza”.Hata hivyo, maafisa wakuu wa uchaguzi nchini Amerika Alhamisi walisema kuwa hakuna ushahidi kwamba kura za Trump zilipotea wala kuibiwa au upigaji wa kura kuvurugwa.

Vile vile, maafisa wa Idara ya Usalama wa Ndani nchini Amerika walisema kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa “salama zaidi katika historia ya nchi hii.”