Mbinu za Uhuru, Raila kukabiliana na malalamishi ya BBI

Na BENSON MATHEKA

Vinara wa mchakato wa kubadilisha katiba nchini, Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, wanatumia mbinu ya kiujanja kutuliza minung’uniko inayotokana na ripoti ya mwisho ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) huku wakihakikisha kuwa wamemfungia nje Naibu Rais William Ruto.

Tangu ripoti hiyo ilipozinduliwa katika ukumbi wa Bomas wiki tatu zilizopita, makundi na viongozi mbalimbali wameelezea kutoridhishwa na baadhi ya mapendekezo na kutaka ichunguzwe upya kabla ya kuwasilishwa kwa kura ya maamuzi.

Tofauti na Dkt Ruto na wandani wake ambao walikuwa wakipinga mchakato mzima wa kubadilisha katiba wakidai una njama fiche, wengi wanaolalamika walitoa maoni yao wakati kamati iliyotwikwa jukumu la kuandika ripoti hiyo ilikuwa ikikusanya maoni kutoka kwa wananchi.

Duru zinasema kwamba Rais Kenyatta na Bw Odinga wameamua kusikiliza wanaodai kwamba maoni yao hayakuzingatiwa lakini sio wale wanaotaka kuchangia maoni mapya ilhali hawakutoa maoni kwa kamati ya watu 14 walioteua kuongoza mchakato huo.

“Ingawa walisema kwamba milango ya mazungumzo kuhusu ripoti hiyo imefungwa, ukweli ni kwamba wanawasikiliza wale walio na maoni ya kuipiga msasa na sio wale wanaoikosoa kabisa. Hawaruhusu mchango kutoka kwa watu walioipinga tangu mwanzo kwa kuwa wanashuku kuwa lengo lao ni kusambaratisha au kuchelewesha mpango mzima,” asema seneta mmoja wa chama cha Jubilee aliye msitari wa mbele kutetea mchakato huo na ambaye hakutaka tutaje jina lake.

Alisema hii ndio sababu vinara hao wamekutana au kukubali malalamishi ya watu walio na ulemavu, jamii ya wafugaji, wabunge na magavana. Viongozi hao walikutana na wabunge mjini Naivasha ambapo walikubaliana jinsi viti vipya za ubunge vitagawanywa. Ripoti ya mwisho ya BBI inapendekeza viti vipya 70 vibuniwe katika bunge.

Rais Kenyatta pia akikutana na vigogo wa kisiasa nchini hasa waliokosoa baadhi ya mapendekezo. Kabla ya kuelekea Italia alikutana na kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ambaye alikosoa mapendekezo kuhusu mahakama, seneti na polisi. Bw Mudavadi pia anataka ripoti hiyo ishughulikie deni la kitaifa ambalo anasema linaweka nchi katika hatari ya kulemaa kiuchumi.

Rais Kenyatta pia alikutana na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Alfred Mutua wa Maendeleo Chap Chap, Charity Ngilu wa Narc na Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya katika juhudi za kujenga uwiano kuhusu ripoti hiyo. Bw Odinga alikutana na viongozi wa jamii za wafugaji na magavana.

Wadadisi wa siasa wanasema mbinu ya vinara hao ya kukutana na watu na makundi mbalimbali yanayolalamika bila kumshirikisha Dkt Ruto inaibua maswali kuhusu kujitolea kwao kuunganisha Wakenya.

“Tumeona mtindo wa kumtenga Dkt Ruto katika mchakato huu kwa sababu wito wake wa mdahalo mpana kuhusu ripoti hiyo ili ipigwe msasa umepuuzwa. Kila wakati akionyesha nia ya kuchangia ripoti hiyo anapuuzwa,” asema mdadisi wa siasa Peter Koech.

Anatoa mfano wa kauli ya Bw Odinga alipokutana na balozi wa China wiki hii kwamba hakuna maoni mapya kuhusu ripoti hiyo yatakayopokelewa ilhali alipokea maoni kutoka kwa jamii za wafugaji ambayo Dkt Ruto aliunga na kutaka makundi mengine na watu kuruhusiwa kutoa yao.

“Ni wazi kuwa vinara hao hawajafunga milango ya kupokea maoni kuhusu BBI mbali wanatumia mbinu ya chini kwa chini kumzima Ruto,” asema Koech.Bw Odinga alisema kwamba ripoti hiyo haitabadilishwa mbali itahaririwa tu. Lakini baadhi ya wadadisi wa siasa na wanaharakati wanatilia shaka hatua hii wakisema huenda mapendekezo tata yasishughulikiwe.

“Mbinu hii haitahalisha mchakato huu ambao unavuruga katiba ya 2010 kwa kupokonya mahakama na Wakenya uhuru na haki zao,” asema mwanaharakati Betreace Akinyi.

Anasema iwapo vinara hao wana nia njema ya kuunganisha Wakenya, kuimarisha ugatuzi na ujumuishi katika serikali, wanafaa kubuni kamati ya wataalamu wa kikatiba kupiga msasa ripoti hiyo.

“Kwa kuwa katiba ni ya Wakenya, sioni sababu ya kukataa maoni kuhusu mapendekezo yaliyo katika ripoti ya mwisho. Kutoa maoni kuhusu mapendekezo ni tofauti na ukusanyaji maoni,” asema.

Wadadisi wanasema kwamba kujitokeza kwa makundi mbalimbali kulalamikia baadhi ya mapendekezo kunaonyesha kuwa inahitaji kupigwa msasa na vinara hao wanafaa kubadilisha mbinu wanayotumia kwa sasa.

“Ili kuwa na mchakato usiopingwa, Rais Kenyatta na Bw Odinga wanafaa kukumbatia uwazi, ili isichukuliwe kwamba wana njama fiche,” asema Koech. Mdadisi huyu anasema madai kwamba ripoti ya mwisho ilibadilishwa na mbinu ambazo vinara hao wanatumia inafanya baadhi ya watu kutilia shaka lengo lao.

Habari zinazohusiana na hii

Acha katambe

Kwa nini tunapinga BBI