• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
VIFO: Joho awahimiza wakazi wa Mombasa wazingatie kanuni za afya nafasi zikikosekana mavani

VIFO: Joho awahimiza wakazi wa Mombasa wazingatie kanuni za afya nafasi zikikosekana mavani

Na WINNIE ATIENO

TAHARUKI imetanda Kaunti ya Mombasa baada ya kubainika nafasi zinakosekana za kuwazika wafu katika makaburi ya umma.

Serikali ya kaunti hiyo inakodolea hatari kufuatia ukosefu wa sehemu za kuzika maiti baada ya makaburi ya umma kujaa ambapo sababu mojawapo ni kuongezeka kwa vifo kutokana na virusi vya corona.

Gavana Hassan Joho ameonya wakazi wenye mapuuza, akiwahimiza wazingatie kanuni za kudhibiti maambukizi ya corona akisisitiza kuwa makaburi yamejaa.

Kulingana na Bw Joho kaburi la umma la Kiziwi, ambalo ndilo kubwa zaidi Kaunti ya Mombasa limesalia na nafasi 20 tu za kuzika maiti.

“Tunawasihi wakazi wa Mombasa wajizatiti kufuata kanuni za kuzuia kuenea kwa corona ili kujikinga wasipate maradhi hatari ya Covid-19. Watu wanakufa sababu ya corona hivyo ninawasihi vaeni barakoa na muoshe mikono mara kwa mara,” alisema Bw Joho kwenye mazishi ya aliyekuwa diwani maalumu Mohammed Hatimy ambaye alifariki kwa sababu ya virusi hivyo.

Bw Joho alilalamika akisema wakazi wanaendelea kupuuza kanuni za kudhibiti virusi hivyo.

Naibu mwenyekiti wa makaburi ya Waislamu ya Kikowani Bw Twalib Khamis aliwaonya wakazi dhidi ya kupuuza kanuni hizo akisisitiza kuwa sehemu za kuzika wafu zinafurika.

Kikowani ndilo eneo la mavani kubwa zaidi la Waislamu, Mombasa.

“Kwa wiki kadhaa zilizopita, tumeshuhudia mazishi ya watu wengi sana. Maiti nyingi inaendelea kuzikwa hapa na tukiendelea na mkondo huu tutakosa sehemu ya kuzika kwani makaburi yatajaa,” alionya.

Haya yanajiri huku wataalam wa kiislamu na madaktari wakiendelea kuonya waumini wao dhidi ya kupuuza maagizo ya wizara ya afya.

Walisema jamii hiyo imesongwa na virusi hivyo ikiwemo vifo kutokana na corona.

Ili kuzuia maambukizi zaidi wamezindua kampeni kuhamasisha jamii hiyo kuhusu hatari ya corona, namna ya kujikinga na umuhimu wa kwenda hospitalini.

Kampeni hiyo pia inanuiwa kukabiliana na dhana potofu kwamba corona haipo Kenya.

Walisema jamii hiyo imeathirika na janga hilo huku wengi wakiendelea kupuuza kanuni kwa kukumbatiana, kuamkuana kwa mikono na kufurika kwenye maharusi.

Mombasa ina zaidi ya vifo 100 na visa 4,000 vya Covid-19.

Dkt Laila Seif alionya jamii hiyo akisema ugonjwa huo umesambaa hadi vijijini huku akiwataka wakazi kufuata kanuni za kujikinga dhidi ya virusi hivyo hatari.

“Gharama ya matibabu ni ghali mno, tafadhalini tutii kanuni ili tujikinge. Wale wenye dalili waende hospitali kwa matibabu. Tuache unyanyapaa,” alisisitiza.

Naye Sheikh Abu Hamza, alisema vifo kutokanan na corona vinaweza kukingwa endapo tu wakazi watafuata kanuni.

“Kuna watu hawaamini ugonjwa huu uko sababu hawajashuhudia katika familia zao. Lakini ile siku watapata kisa kimoja, wataamini, hii ni dhana potovu. Ama tufuate kanuni na tuwe salama au tufanye tunavyotaka na tuangamie,” alionya.

You can share this post!

Visa vya watu kujaribu kujitoa uhai na wengine kujitia...

Mwanafunzi afariki kutokana na corona Mumias