• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
GWIJI WA WIKI: Emily Gatwiri

GWIJI WA WIKI: Emily Gatwiri

Na CHRIS ADUNGO

MAFANIKIO ni zao la bidii, imani na stahamala.

Usipoteze dira ya maono yako maishani hata unapokumbana na changamoto. Kuwa na matumaini hata pale ambapo mambo yanakwenda kinyume na matarajio yako na uvute subira kwa imani kwamba siku njema itafika.

Mtangulize Mungu katika kila hatua ya maisha, kuwa radhi kuwajibikia matendo yako na ukipende hicho unachokifanya kwa moyo wa dhati.

Kipimo cha mafanikio ya mtu si utajiri wa mali na wingi wa fedha; bali ni ukubwa wa alama zenye kumbukumbu nzuri anazoziacha katika nyoyo na nafsi za wale anaowatumikia au kuwaongoza.

Ndoto zako haziwezi kabisa kutimia iwapo hutajitolea kuzifanyia kazi. Amua pa kuanzia baada ya kufanya maamuzi sahihi. Jitume bila ya kutafuta visingizio. Amini unaweza na usichoke kutafuta!

Mungu alipokuumba, alikupa kipaji na uwezo wa kukitumia vyema. Kulaza damu na kushindana na watu ni upumbavu. Badili mtazamo wako na ujiwekee malengo mapya ya mara kwa mara.

Huu ndio ushauri wa Bi Emily Gatwiri – mwandishi chipukizi wa Fasihi ya Kiswahili ambaye kwa sasa ni mwalimu katika Shule ya Msingi ya Sukari Presbyterian Academy, eneo la Kahawa Sukari, Kaunti ya Kiambu.

MAISHA YA AWALI

Emily alizaliwa mnamo Mei 2, 1989, katika kijiji cha Ntua, eneo la Tigania Magharibi, Kaunti ya Meru. Ndiye mwanambee katika familia ya watoto watatu wa Bw Zaverio Baariu na Bi Benedicta Naita. Nduguze Emily ni Yvonne Mukiri ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule ya Upili ya St Francis Mang’u, Kiambu na Victor Muriithi anayesomea katika Shule ya Msingi ya Ahadi Presbyterian, eneo la Kenyatta Road, Kiambu.

Emily pia ni mama wa wavulana wawili – Lameck Mwangi, 6, na Alex Mwenda, 4. Wote hao wanasomea katika Shule ya Sukari Presbyterian.

Mnamo 1996, Emily alijiunga na Shule ya Msingi ya St Kizito, Kaunti ya Isiolo. Anakumbuka alivyokuwa chini kimasomo wakati huo.

“Nikiwa mwanafunzi wa Darasa la Kwanza, sikujua kusoma kabisa. Sikung’amua chochote ila kwa msaada wa mwalimu wangu, Bi Ntoribi aliyekuwa akisalia nami shuleni ili anisaidie kusoma baada ya wenzangu kuondoka na kurejea nyumbani adhuhuri.

“Bi Ntoribi alikwenda nami nyumbani kwake mara kwa mara kwa masomo ya ziada. Upendo wake kwangu ulinitia ari ya kuchangamkia masomo. Kuanzia hapo, historia yangu iliandikwa upya, nikawa miongoni mwa wanafunzi bora zaidi darasani.”

Kutokana na kumbukumbu hiyo, Emily anaamini kuwa kila mwanafunzi ana uwezo wa kufaulu vyema masomoni. Anakiri kuwa mwalimu wake angekosa kumwamini, kumwelekeza ipasavyo na kumpokeza malezi bora ya kiakademia, basi masomo kwake yangesalia usiku wa kiza.

Mbali na Bi Ntoribi, mwingine aliyemchochea na kumhimiza Emily kujitosa katika ulingo wa ualimu ni Bi Saba aliyemfundisha kuanzia Darasa la Nne hadi Darasa la Nane. Ingawa Emily hakuwa na maazimio ya kuwa mwalimu hapo awali, alijenga upendo wake katika taaluma hiyo hatua kwa hatua, na amekuwa na msukumo wa kujiboresha kila uchao.

Baada ya kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika Shule ya Msingi ya St Kizito mnamo 2003, Emily alijiunga na Shule ya Upili ya Mfariji Girls iliyoko Mutuati, Kaunti Meru mnamo 2004. Alisomea huko kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kuhamia Shule ya Upili ya Akithii Girls, Tigania Magharibi. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mwishoni mwa 2007.

Kati ya walimu waliomtia ilhamu ya kuchangamkia masomo ya lugha ni Bi Victoria na Bi Kaibung’a ambao walimtanguliza vyema katika Fasihi ya Kiingereza na kutambua utajiri wa kipaji chake katika uandishi wa kazi bunilizi. Mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kwamba Kiswahili ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi; ni Bi Makena Muriungi.

Bi Victoria alimpigia Emily mhuri wa kuwa mwandishi stadi wa kazi za kitaaluma na kumpa motisha ya kujitosa kikamilifu ulingoni na kupiga mbizi katika bahari pana ya utunzi na uhakiki wa fasihi baada ya kutathmini mswada wake wa kwanza wa riwaya ya Kiingereza mnamo 2014.

Emily alisomea ualimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Murang’a kati ya 2008 na 2010. Ilikuwa hadi 2015 ambapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea shahada ya ualimu (Kiswahili na Dini).

UALIMU

Kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya Sukari Presbyterian anakofundisha kwa sasa, Emily aliwahi kuwa mwalimu katika shule za Juja St Peters, Tulivu Junior Academy, North Riara Ridge na Ahadi Presbyterian.

Amewahi pia kuwa mkutubi msaidizi katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Thogoto, Kiambu kati ya 2012 na 2014. Akiwa huko, alipata fursa ya kuwa karani wa Baraza la Mitihani ya Kitaifa nchini Kenya (KNEC) kati ya 2012 na 2013.

UANDISHI

Emily alishiriki uandishi wa vitabu kwa minajili ya Mtaala Mpya wa Umilisi (CBC) mnamo 2019. Tangu wakati huo, ameandika vitabu vingi vya hadithi za watoto ambavyo vitachapishwa hivi karibuni. Ameshirikiana pia na waandishi chipukizi na waliobobea kuchapisha antholojia mbalimbali za hadithi fupi.

Hadithi yake ‘Chovya Chovya’ ilichapishwa na kampuni ya The Writers’ Pen Publishers, Eldoret katika mkusanyiko wa ‘Shaka ya Maisha na Hadithi Nyingine’ mnamo Julai 2020.

Emily ndiye mwandishi wa hadithi ‘Kosa La Baba’ katika katika diwani ya watoto ya ‘Kuku Ameshinda Kura na Hadithi Nyingine’ iliyofyatuliwa na kampuni ya Williams Publishers, Kisumu mnamo Septemba 2020.

Kabla ya Chania Publishers kumchapishia hadithi ‘Jambazi wa Chuoni’ katika antholojia ya ‘Siwezi Tena’ na Hadithi Nyingine mnamo Oktoba 2020, Emily alikuwa amechangia mashairi katika ‘Diwani ya Maradhi’ iliyotolewa na The Writer’s Pen mnamo Agosti 2020.

Sanaa ya uandishi ilianza kujikuza ndani ya Emily tangu akiwa mtoto mdogo. Babaye mzazi alikuwa akimnunulia magazeti kila siku na kumuongoza kushiriki mashindano mbalimbali ya uandishi kwenye kumbi za watoto magazetini. Pia alimnunulia vitabu vingi vya hadithi vilivyompa kariha ya kuandika insha zilizovutia na kustaajabisha walimu na wanafunzi wenzake kwa ufundi wa lugha na ubunifu wa kipekee.

Kati ya waandishi, wasomi na wataalamu waliomwamshia Emily ari ya kuzamia uandishi wa vitabu ni Bw Mutahi Miricho, Bw Sam Mbure na Bw Moses Murithi Murega ambaye ni mhariri katika Shirika la Uchapishaji la Kenya Literature Bureau (KLB).

Weingine ni Bw Kinyanjui Kombani, Bw Richard Ondoli Amunga, Bw Angira O. Angira, Hussein Kassim, Timothy Omusikoyo Sumba na Bw Gabriel Dinda ambaye ni mwanzilishi na mkurugenzi wa Shirika la Writers’ Guild.

You can share this post!

MATHEKA: Serikali haijaonyesha nia ya kuzima uagizaji sukari

Uhispania yafunza Ujerumani kusakata gozi la UEFA Nations...