MWANAMUME KAMILI: Kipungu hawezi kuenda safari moja na mwewe!
Na DKT CHARLES OBENE
MWANZONI mwa wiki hii nikiwa safarini, nilibahatika kudakia mazungumzo yaliyojiri kwenye mjadala uliopeperushwa redioni.
Wajua tena ada ya hawa watangazaji wenye “jambo” kutania na kufanyia maisha mzaha sisemi kukuza vijimambo vikawa mambo! Wamebobea si haba watu hawa kutuvunja mbavu kwa kuangazia visa na vituko vya ajabu. Walichagua mada tata kuhusu mwanamume na pesa. Wasikilizaji walihitajika kutoa maoni na kuchangia kihalisia iwapo “mwanamume wa Kiafrika asiye na pesa anastahili heshima na mapenzi ya dhati kama mwanamume kamili!”
Kilichonishangaza mno ni idadi ya wanawake waliopiga simu na kuwasilisha hisia zao redioni. Wote waliungama kwa sauti moja kwamba mwanamume asiye na pesa sio mume! Hastahili heshima wala mapenzi. Wanaume nao waliopiga simu waliteta mno na kuwahukumu wanawake “wanaoketi zuliani na kusubiri kuletewa pesa sebuleni!” Tetesi za madume zililenga mno kuhuisha ile dhana kwamba wanawake wa leo wanafuata pesa badala ya kufuata mapenzi.
Hapo ndipo navua heshima na kutangaza wazi kwamba afadhali mtu kufuata pesa anazoweza kuzishika, akaziona zikamfaa! Nawahamasisha nyie wanawake mnaokemewa! Fuateni pesa! Fuateni hadi kuzipata popote mtakapokutana nazo. Angalau pesa zinawanunulia poda, wanja, herini, kanchiri, majozi ya viatu na mapambo si haba. Na mapenzi je? Wangapi wamefuata mapenzi wakakutana ana kwa ana? Sijawahi kuona maduka ya jumla yanayouza bidhaa kwa malipo ya “mapenzi!” Vito vya mwanamume ni viwili – pesa na jina. Hamna budi kujenga maghala kuhifadhi hivi viwili. Pesa na jina.
Msijekufa moyo kwa kauli yangu enyi wanaume mnaofuata mapenzi. Dunia ni huru huria na kila mtu anaruhusiwa kufuata, kutafuta na kulimbikiza asichokua nacho! Fuateni mapenzi nyie gumegume wa leo lakini acheni wanawake wakatafute pesa. Mwisho wa siku tutakadiria na kuona nani mpumbavu!
Binafsi, najitahidi sana kila mara kujizuia kutia dole mzingani kwa hofu ya usena wa nyuki. Kwa hamasa na hamaki iliyonijaa kifuani, nitavunja kingo na kuta zote na kuyatoa yanayonikaba kooni. Kwanza kabisa, nawahongera na kuwapongeza wanawake waliokwisha janjaruka na kuerevuka kiasi kwamba wanajituma kimaisha pasipo kutegemea mfuko wa mwanamume! Kila mtu mwenye akili ana wajibu wa kipekee kuzitumia akili hizo kwa manufaa ya jamii na familia. Si mwanamume si mwanamke.
Pili, mwanamume lazima awe mwanamume kwa maana halisi ya mwanamume pasipo kuzingatia uzawa wake. Awe barani Afrika, Uropa, Marekani, Asia na maeneo ya kati mashariki mwa dunia, mwanamume hana budi kuwa mwanamume kamili. Kama ndevu ni mume, hata mbuzi anazo! Kama majozi ya viatu ni ishara ya mwanamume, hata farasi wanavishwa. Kama nguo nadhifu na mabango ya dhahabu ndizo ishara za mwanamume, hata maiti wanavishwa! Kuishi kama bwege – mwanamume fukara mfano wa fuko ni udunishaji mkubwa wa hadhi ya mume. Tatu, hakuna mume aliyetia bidii kuchuma mali, aliyeekeza sarafu na jasho lake pema, aliye dhibiti ubadhirifu na mwishowe akafa fukara. Hakuna wala hatakuwepo.
Nne, hawa gumegume tunaowasasavua ama tunaowavua katika baharí ya walevi na kuwaita wanaume ndio tishio kubwa wenda wakasambaratisha imani ya wanawake katika ndoa. Mwanamume asiye na pesa ama uwezo kukuza na kulea familia anaitakia nini? Sijawahi kumwona ndovu anakula mawe kwa kuwa ana uwezo kuyandondoa na kuyatoa utumboni. Iweje mwanamume mwenye akili razini akatafuta kuoa mtoto wa mtu huku anajua wazi hana hanani? Jamani mbona kutafuta watoto wa watu, kuwarundika, kuwavumbika kiume na mwishowe kuwaachia mizigo kujilea na kujitunza?
Tano, nanyi wanawake wa leo mwanishangaza vilevile. Mnakwenda tafuta nini katika maisha ya watu ambao hata nyuso zao kunawa wanaiona kama kazi ya sulubu. Mnakwenda tafuta nini maishani mwa watu wasioweza hata kujilisha? Mlivyo wenye akili na bidii kazini na chumbani, mbona kujifinya kwenye mikeka kuolewa na magogo ya wanaume wasiojua hata maana ya mwanamume? Ndio nyie mnaolalama redioni.
Dunia ilivyojaa pomoni wanaume wenye bidii na chudi, lakini bado kuna watoto wa watu wanaolalia ndoto na kuamka asubuhi kufuata mapenzi kutoka vitanda vya walahoi waliokataa katakata kukomaa na kuwa wanaume kamili. Mimi nikijua maana na hadhi ya mwanamke mwema, inanijuzu kujituma na kumpa angalau kibanda chake, kwenye ardhi yake – kama kulala anaweza lalia miguu juu!
Wanaume wa leo wanawaharibia wawake muda bure. Isitoshe, hawa vimwana wanaojisabilia mikononi mwa malofa ndio wao hao wanaolalama juu ya ubwege wa wanaume wa leo. Nataka kuwajuza kwamba bwege ndiye hujua bwege. Kipungu hawezi kwenda safari moja na mwewe!