Chebukati aanzisha juhudi za kunusuru IEBC
KENNEDY KIMANTHI na PATRICK LANG’AT
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati ameanzisha juhudi za kuokoa tume hiyo isiongozwe na vyama vya kisiasa inavyopendekeza ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).
BBI inapendekeza makamishna wapya wateuliwe baada ya kupendekezwa na vyama vikuu vya kisiasa huku pia ikitaka wafanyakazi wote kwenye tume wapigwe msasa.
Hata hivyo, Bw Chebukati amekuwa akisisitiza hawabanduki hadi muhula wao wa kuhudumu ukamilike huku akipigania tume hiyo ipewe uhuru wa kutumia fedha zake bila bajeti yake kudhibitiwa.
Makamishina wa IEBC wamekuwa kikaangioni wakidaiwa kuvuruga matokeo ya uchaguzi wa 2017.
Hata hivyo, Bw Chebukati anataka tume hiyo ilindwe kutoka kwa uvamizi wa wanasiasa ili imakinikie utendakazi wake.
“Vyama vya kisiasa kuruhusiwa kuwateua makamishina wa IEBC, kutaathiri utendakazi wake. Hii ni kwa sababu siasa za Kenya huwa zimejaa ukabila na baadhi ya vyama huwa hata havidumu kwa muda wa miaka mitano,” akasema Bw Chebukati kwenye chapisho gazetini wiki hii.
Mnamo Jumatano, chama cha ODM kilikashifu hatua ya IEBC kupinga makamishna wa tume kuchaguliwa na vyama vya kisiasa.
“Uchaguzi wa 2002 ambao ulikuwa na uwazi mkubwa uliendeshwa na wawakilishi wa vyama vya kisiasa kama makamishna. Walioko sasa wanapinga mabadiliko kwenye tume ili kulinda kazi zao ilhali wamekuwa wakivuruga kura miaka ya nyuma,” akasema Katibu wa ODM Edwin Sifuna.
Hata hivyo, Bw Chebukati alisisitzia kuwa kuvunjwa kwa IEBC kila baada ya uchaguzi si suluhu kwa usimamizi unaodaiwa kuwa mbaya kwenye chaguzi hizo.