• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Wajane wa Murunga wataka wapewe mwili wazike

Wajane wa Murunga wataka wapewe mwili wazike

Na RICHARD MUNGUTI

WAJANE wawili wa aliyekuwa Mbunge wa Matungu sasa wanaitaka mahakaama iamuru wapewe mwili wa mume wao wakamzike Novemba 28, 2020 huku wakiomba mlalamishi aweke dhamana ya Sh10milioni kortini kugharamia kesi na mazishi.

Katika kesi waliyoshtaki Ijumaa alasiri, Bi Christabel Jane na Grace wanaomba korti ifutilie mbali agizo la kusitisha mazishi hayo wakisema “itakuwa ni gharama kubwa mazishi hayo kuvurugwa.”

Mahakama iliamuru mochari ya Lee Funeral isiachilie mwili wa Murunga hadi kesi iliyoshtakiwa na mke wake wa tatu Agnes Wangui Wambiri isikizwe na kuamuliwa.

Christabel na Grace wamesema “ kamwe hawamjui Agnes Wangui Wambiri na watoto wake wawili.”

Wajane hao wanadai “ni wao tu wake rasmi wa mwanasiasa huyo na madai ya Wangui ni hekaya tupu isiyoweza kuaminika na kamwe haina mashiko kisheria.”

Kupitia kwa wakili Patrick Lutta , wake hao wanaomba mahakama imwamuru Wangui aweke dhamana kortini ya Sh10milioni kugharamia mazishi na ada za kuhifadhi mwili katika mochari ya Lee.”

Wawili hao wanasema tayari gharama kubwa imepatikana na kuhifadhi mwili wa mume wao katika mochari.

“Bunge la kitaifa pamoja na familia ya marehemu imepata gharama kubwa kulipia ada ya kuhufadhi mwili katika mochari,” asema Bw Lutta katika kesi aliyowasilisha chini ya sheria za dharura.

Wakili huyo amependekezea mahakama sampuli kutoka kwa mwili wa Murunga zitolewe na kupelekwa kwa maabara kufanyiwa uchunguzi wa DNA kubaini ikiwa marehemu aliwazaa watoto wawili na Wangui.

“Endapo itabainika ni uwongo Murunga hakuwazaa watoto hao wawili na Wangui itakuwa ni fedheha kubwa,” amedokeza Bw Lutta.

Wajane hao wanasema kulingana na mila na desturi za Waluhya marehemu anapasa kuzikwa katika boma ya mke wa kwanza.

Pia wanasema wanapata gharama kubwa kuendeleza matanga katika boma zote za marehemu jijini Nairobi na kaunti ya Kakamega.

Wajane hao wanaomba korti iamuru kesi hiyo isikizwe Novemba 24 2020 ndipo maagizo yatolewe mazishi yaendelee Novemba 28 katika eneo la uwakilishi bungeni la Matungu.

Mnamo Novemba 18 hakimu mkazi Bi A N Makau aliamuru mazishi ya Murunga yasiendelee hadi kesi iliyoshtakiwa na Wanguo isikizwe na kuamuliwa.

Bi Makau aliamuru sampuli zitolewe katika mwili wa Murunga na kupelekwa kufanyiwa ukaguzi wa DNA kubaini ikiwa ndiye baba wa watoto wawili anaodaiwa aliwazaa na Wangui.

Watoto hao wako na umri ulio chini ya miaka 10. Kifungua mimba alizaliwa 2013 na kitinda mimba alizaliwa 2017.

Bi Makau aliratibisha kesi iliyowasilishwa kortini na wakili Danstan Omari na kuagiza isikziwe Nobvemba 26, 2020.

Mahakama ilisema kuwa kesi ya Wangui iko na mashiko kisheria kwa vile inahusisha masuala ya watoto.

“Masuala na haki za watoto hazikomi mzazi anapoaga. Sitaendelea kushinishwa kwa walio salia hadi watoto hao watakapofikia umri wa kujimudu,” Bw Omari alimweleza Bi Makau.

Mahakama iliombwa iamuru watoto hao pamoja na mama yao waruhusiwe kushiriki katika mipango na mazishi ya marehemu.

“Mlalamishi pamoja na watoto wake wanataka wahusishwe katika mipango ya mazishi ya Murunga,” alisema Omari.

Wakili huyo aliomba mahakama isitishe mazishi hayo hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

You can share this post!

Mipango ya mazishi ya Murunga bado yaendelea

Ukosefu wa hela umeeneza corona kwenye kaunti –...