Mourinho amzidi Pep ujanja na kuongoza Spurs kudhibiti kileleni mwa jedwali la EPL
Na MASHIRIKA
USHINDI wa 2-0 ulisajiliwa na Tottenham Hotspur dhidi ya Manchester City mnamo Novemba 21, 2020, ukiwaweka kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mara ya kwanza baada ya miaka sita.
Matokeo hayo yalimvunia kocha Jose Mourinho tija na fahari zaidi baada ya kumzidi maarifa mpinzani wake wa tangu jadi, Pep Guardiola.
Son Heung-min aliwaweka Spurs kifua mbele katika dakika ya tano baada ya kukamilisha krosi ya kiungo Tanguy Ndombele. Beki Aymeric Laporte alidhani alikuwa amesawazishia Man-City katika dakika ya 17 ila bao lake likafutiliwa mbali na refa baada ya marejeleo ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba fowadi Gabriel Jesus alikuwa ameunawa mpira kabla ya kujazwa kimiani mwa Spurs.
Licha ya Man-City kumiliki asimilia kubwa ya mpira na kutamalaki mchezo mzima, Spurs walisalia imara katika ngome yao na kudhibiti makali ya wageni wao vilivyo.
Ilikuwa hadi dakika ya 65 ambapo Spurs walifungiwa bao la pili kupitia kwa kiungo Giovani lo Celso aliyemwacha hoi kipa Ederson Moraes sekunde chache baada ya kuingizwa uwanjani katika kipindi cha pili kujaza nafasi ya Ndombele.
Pigo zaidi kwa Spurs mwishoni mwa mechi hiyo ni jeraha alilolipata kiungo Toby Alderweireld.
Spurs kwa sasa wanajivunia mojawapo ya safu bora zaidi za mbele katika soka ya EPL kutokana na kasi na wingi wa maarifa ya Son ambaye anazidi kushirikiana vilivyo na Gareth Bale na nahodha Harry Kane. Ubora wa watatu huo umechangiwa zaidi na uwepo wa sajili mpya Pierre-Emile Hojbjerg aliyesajiliwa na Spurs mwanzoni mwa muhula huu kutoka kambini mwa Southampton.
Kwa upande wao, mashabiki wa Man-City walilalamikia pakubwa mbinu za ukufunzi wa kocha Pep Guardiola aliyeteua kuwasaza Raheem Sterling na Sergio Aguero kwenye benchi kabla ya kuwaleta ugani katika kipindi cha pili.
“Huenda tusisalie kileleni mwa jedwali kwa kipindi kirefu kirefu. Lakini si rahisi kushinda Man-City ambao pia wana kiu ya kutwaa ubingwa wa taji la EPL msimu huu. Japo maazimio yetu si kunyanyua ufalme, tuna nia ya kusajili ushindi katika kila mojawapo ya mechi,”akasema Mourinho.
Alama 12 ambazo Man-City wamejizolea kutokana na mechi nane zilizopita ndizo chache zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kujitwalia katika hatua kama hii kwenye kampeni za EPL tangu 2008-09.
Aidha, mabao 10 ambayo Man-City wamefunga ndiyo idadi ndogo zaidi kwa miamba hao wa soka ya Uingereza kuwahi kupachika wavuni baada ya mechi nane tangu 2006-07.
Ilikuwa mara ya kwanza tangu Oktoba 2016 kwa Tottenham kusajili ushindi dhidi ya Man-City mara mbili mfululizo ligini.
Man-City kwa sasa wanajiandaa kuwaendea Olympiakos ya Ugiriki kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 25, 2020 huku Tottenham wakiwaalika Ludogorets ya Bulgaria kwenye Europa League mnamo Novemba 26, 2020.
Baada ya hapo, Man-City watawaalika Burnley kwa gozi la EPL ugani Etihad kabla mnamo Novemba 28 siku moja kabla ya Spurs kushuka dimbani kumenyana na Chelsea uwanjani Stamford Bridge.