Morderna kuuza chanjo ya corona kwa bei nafuu
CHARLES WASONGA na MASHIRIKA
KAMPUNI ya dawa ya asili ya Amerika, Moderna, imetangaza kuwa itauza chanjo iliyovumbua kwa bei ya kati ya Sh2,700 na Sh4,000 kwa kila kipimo, kulingana na kiasi ambacho kila nchi itaagiza.
Hii ni kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Stephen Bancel akinukulikiwa na gazeti la kila wiki nchini Ujerumani, “Welt am Sonntag (WamS)”.
“Chanjo yetu haitakuwa ghali kwani itagharimu kati ya dola 10 na dola 50,” akasema.
Mnamo Jumatatu, afisa mmoja wa Tume ya Ulaya (EC) alitaka kuweka mkataba na kampuni ya Moderna ili iweze kuiuzia milioni kadha za vipimo vya chanjo yake kwa bei ya Sh2, 700 kwa kila kipimo.
Moderna imesema kuwa chanjo yake ambayo imefanyiwa majaribio imegunduliwa kuwa na ubora wa kima cha asilimia 94.5 katika kuzuia Covid-19.
Chanjo hiyo sasa ni ya pili kuleta matumaini katika juhudi za kusaka tiba ya homa hii hatari.
Majuma mawili yaliyopita kampuni kubwa ya dawa kutoka Amerika Pfizer na mshirika wake kutoka Ujerumani BioNTech zilidai kuvumbua chanjo ambayo ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kwa kiwango cha asilimia 95.
Kampuni ya Moderna ina makao yake makuu jijini Cambridge katika jimbo la Massachusetts.
Hata hivyo, Waziri wa Afya nchini Kenya Mutahi Kagwe ametilia shaka uwezo wa chanjo hiyo kudhibiti janga hilo akionya dhidi ya Wakenya kutumiwa kufanyia majaribio chanjo ambazo usalama “wao ni wa kutiliwa shaka.”
“Binafsi sina imani na chanjo hiyo ambayo nilisikia imevumbuliwa na kampuni ya Pfizer. Mbona iwe kwamba inapewa mtu kuzuia asiambukizwe virusi? Kwani watajuaje ikiwa nitapata virusi hivyo au la?” Bw Kagwe akauliza alipofika mbele ya Kamati ya Seneti.