• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 8:55 AM
TAHARIRI: Kenya isilale kufufua uchumi

TAHARIRI: Kenya isilale kufufua uchumi

KITENGO CHA UHARIRI

SERIKALI sasa inafaa ianze kuweka mikakati thabiti ambayo itasaidia kufufua uchumi haraka iwezekanavyo.

Kufikia sasa, mipango ambayo tumeona ikipewa uzito ni ile ya kunusuru wananchi na wafanyabiashara wasiangamie kwa hasara zilizosababishwa na janga la corona.

Ijapokuwa tumesikia kuhusu mikakati ya kurudisha hali ya kawaida baada ya janga hili kuondoka, inahitajika mengi zaidi yafanywe.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya biashara (UNCTAD) tayari limeonya kuwa mataifa maskini yataendelea kuathirika kiuchumi hata baada ya janga la corona kupata suluhisho.

Suluhisho linalosubiriwa kutatua janga lililopo ni chanjo ambayo itafanikiwa kuepusha maambukizi ya virusi vya corona kwa binadamu.

Katika wiki za hivi majuzi, kampuni kadhaa zinazohusika katika utafutaji wa chanjo zimeeleza matumaini ya kupata chanjo ambazo zinaweza kuzuia virusi hivyo kwa zaidi ya asilimia 90.

Ijapokuwa matangazo hayo yanaleta matumaini, ripoti iliyotolewa wiki iliyopita na UNCTAD imesisitiza kuwa athari tunazoona leo zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu hata baada ya chanjo kuanza kutumiwa rasmi.

Nchi maskini ziko taabani kwa vile hata kupata chanjo inayotarajiwa haitakuwa rahisi.

Wataalamu tayari wameonya kwamba nchi tajiri kama vile Amerika na mataifa ya Ulaya yameagiza mabilioni ya dozi za chanjo ambazo hata hazijakamilika kutengenezwa.

Kwa msingi huu, kuna hatari ya nchi maskini au zile zinazoendelea kustawi kama vile Kenya kubaki nyuma baada ya chanjo kupatikana.

Serikali lazima ianze sasa kutafuta kila mbinu ya kuhakikisha athari zinazoshuhudiwa hazitadumu kwa muda mrefu wakati mataifa mengine yatakapokuwa yanajifufua kwa kasi.

Jambo la kwanza linalohitajika ni kutumia wataalamu wa masuala ya kiuchumi na kijamii kutoa mwelekeo mwafaka ambao utatuendeleza mbele.

Kando na hayo, inafaa taifa hili lizingatie kufanya utathmini kikamilifu kuhusu ushirikiano wake na mataifa ya kigeni na pia uanachama wake katika mashirika mbalimbali ya kimataifa.

Utathmini huu ubainishe ushirikiano ambao unaweza kutufaa kuendelea mbele, na kutenga yale ambayo huenda yakawa mzigo kwetu katika miaka ya usoni.

You can share this post!

Mswada waibua kiwewe kwa walanguzi wa dawa

OMAUYA: Wakati wa Museveni kuondoka sasa umefika