Dereva wa lori lililoanguka Viwandani aokolewa
Na SAMMY KIMATU
WIKI moja baada ya mtu mmoja kufariki papo hapo baada ya kugongwa na matatu iliyokuwa ikienda kwa kasi eneo la Viwanda kaunti ya Nairobi, ajali nyingine ilitokea Jumatatu.
Dereva wa lori lililokuwa likisafirisha chakula cha kuku aliokolewa bila kuumia baada ya lori lake kuanguka.
Polisi walisema gari hilo lilikuwa lenye nambari ya usajili KBV 060C aina ya Mitsubitshi FH lenye rangi nyeupe.
Akizungumza na Taifa Leo katika eneo la tukio, dereva huyo, Bw Fauzal Mohammed, 23, alisema lori hilo lilipinduka alipojaribu kuingia barabara kuu ya Entreprise kwenye makutano yanayounganisha mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba katika kaunti ndogo ya Starehe.
“Nilikuwa nikijaribu kupiga kona kwenye mtaa wa mabanda wa Kayaba na maramoja gari likaanguka na upande wa kushoto. Ni mahali ambapo mwenye kandarasi ya barabara hiyo ameacha kazi ambayo haijakamilika na ambapo ni sehemu iliyo na muinuko. Hata hivyo, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa hai, ” Bw Mohammed akasema.
Maafisa wa polisi wa trafiki walikuwa na kazi ya ziada kudhibiti magari huku msongamano wa magari ukionekana zaidi ya kilomita mbili.
Ajali hiyo ya asubuhi, ilisababisha msongamano wa magari katika eneo nzima ya Viwanda lenye shughuli nyingi haswa katika barabara za Lunga Lunga, Entreprise na Likoni, Isitoshe, barabra hizo ni kitovu cha eneo la Viwanda.
Tukio hilo lilikwamisha biashara nyingi. Vilevile, Ilichukua wafanyakazi wa kukokota magari zaidi ya saa moja kurudisha lori hilo barabarani. Kadhalika, karibu na eneo la ajali kuna sehemu ya watembeao kwa miguu ambayo haijapakwa rangi na kuripotiwa watu wengi wamegongwa na magari.
Waliohojiwa walisema mwanakandarasi hajapaka rangi eneo la kuvukia karibu na mzunguzo wa barabara ya Kampala.
“Tunawauliza viongozi kuhakikisha mahali pa watu kuvukia wakitembea kwa miguu pamepakwa rangi ndiposa tuzuie ajali zaidi hasa katika steji ya Kaiyaba ambapo kuna mashimo na miinuko ukiunganisha barabara kuu ya Entreprise,” Bw Onesmus Kaleli, afisa wa Nyumba kumi katika mtaa wa mabanda wa Kayaba akanena.