KINA CHA FIKIRA: Jitahidi ule jasho lako, vya wengine vitakusakama
Na WALLAH BIN WALLAH
MAISHA si mteremko.
Ni safari ngumu kama kuukwea mlima! Lakini unavyozidi kuukwea mlima ndivyo unavyosonga zaidi juu kileleni. Lazima ujitahidi na uvumilie ndipo ufanikiwe! Maisha ni magumu na kuishi si rahisi. Unapaswa kuwa mgumu! Ukaze moyo na uutumikishe ubongo ufanye kazi. Akili inayofanya kazi hailali. Akili isiyolala ndiyo inayoleta mali tunu! Mali halali hupatikana kwa akili ambayo hailali. Usitafute mali haramu kwa njia ya mkato! Njia ya mkato ikikatika huyakata maisha yakaisha! Hivyo ndivyo Mzee Bongombili alivyomuusia mjukuu wake Tekemoja!
Miaka mingi baadaye tangu Mzee Bongombili alipoaga dunia, Tekemoja alikumbwa na njaa. Akachukua upanga kuenda msituni kukata kuni akauze kijijini apate pesa anunue chakula! Jua lilikuwa kali sana! Alipokuwa akikata kuni alisikia sauti dhaifu ikimwita, “Eee, kijana, njoo!” Alipotazama kushoto alimwona mzee mkongwe mwenye nywele timtimu za mvi! Alimsogelea akamsalimia kwa huruma, “Shikamoo babu?” Mzee aliitikia kwa unyonge, “Marahaba mjukuu wangu!” Kisha mzee akamwonyesha Tekemoja unyayo wake uliokuwa umedungwa na mwiba mkubwa! Tekemoja alishika mwiba akauvuta kuutoa! Mzee alihisi uchungu sana! Mwiba ulipotoka damu ilichirizika! Tekemoja alirarua kipande cha shati lake akalifunga jeraha kuzuia damu! Babu alipata nafuu akatamka, “Asante sana mjukuu wangu lakini nina njaa na kiu! Tangu mwiba huu uliponidunga siku tano sijala chochote!”
Tekemoja alitoa kibuyu cha maji na vipande vya muhogo uliochemshwa kutoka katika mkoba wake akampa mzee akala akanywa maji! Babu alipata uhai upya! Akamwambia Tekemoja, “Hali ni ngumu na maisha ni magumu sana! Lakini binadamu asikate tamaa wala asitafute kuishi kwa kutumia njia haramu! Na muhimu zaidi ni kwamba, heri kuwe na ukame wa mazingira badala ya ukame wa wema, utu na uadilifu! Kumbuka, wema hauozi!” Baada ya kusema hivyo, Babu alimwonyesha Tekemoja ng’ombe aliyefungwa kwa kamba kwenye shina la mti kando. Akasema, “Umchukue ng’ombe yule! Utakuwa ukimkama kila siku upate maziwa mengi ya kunywa na kuuza! Lakini mwiko ni kwamba, wewe au mtu yeyote asipitie upande wa nyuma ya ng’ombe huyo!” Mzee akatoweka!
Tangu siku hiyo Tekemoja akawa muuzaji maarufu wa maziwa akapata pesa nyingi! Lakini usiku mmoja wezi walikuja wakamwiba ng’ombe wake! Alipoamka asubuhi alisikitika sana. Kumbe waliomwibia ng’ombe walikuwa rafiki zake wakubwa, Seko na Sako! Huko Sako alipopita nyuma ya ng’ombe ili amkame alipigwa teke mdomoni akang’olewa meno kumi! Seko alipojaribu kumwinua Sako amtoe nyuma ya ng’ombe, alipigwa teke kichwani akafa pale pale!
Ndugu wapenzi, hata kama maisha ni magumu, lakini ujitahidi ule jasho lako! Usithubutu kupora mali ya wengine!