Corona yasukuma milioni 2 kwa dhiki
Na PAUL WAFULA
JANGA la corona limesukuma Wakenya milioni mbili kwa orodha ya walio maskini kwa kiasi kwamba hawawezi kumudu mahitaji ya kimsingi, ripoti ya Benki ya Dunia imefichua.
Hatua hii ni pigo kwa juhudi za kumaliza umaskini ambazo Kenya ilikuwa imepiga kwa miaka mitano huku idadi ya watu wasio na ajira ikiendelea kuongezeka.
Ripoti hiyo, ambayo sasa inathibitisha kwamba uchumi wa Kenya umeathirika vibaya, inakadiria kuwa utadorora zaidi kwa asilimia moja mwaka huu.
Tayari, uchumi umedorora kwa asilimia 5.7 katika robo ya pili ya mwaka huu na utahitaji kustawi kwa kiwango kikubwa katika muda uliosalia kubadilisha hali jambo ambalo halitawezekana katika mazingira ya sasa.
“Kote ulimwenguni, uchumi unatarajiwa kudorora 2020, na athari hizi mbaya zinaweza kuenea hadi Kenya,” inasema ripoti ya hali ya uchumi nchini Kenya ya Novemba 2020.
Ripoti inaongeza kuwa janga hili limefuta na kufifisha mafanikio ambayo Kenya ilikuwa imepiga kuangamiza umaskini kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
“Janga hili limeongeza umaskini kwa asilimia nne (watu milioni mbili zaidi) kwa kuathiri vibaya maisha yao, kupungua kwa mapato yao na kukosa ajira,” inaeleza ripoti iliyotolewa Jumatano.
Inasema kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimeongezeka maradufu hadi asilimia 10.4 katika robo ya pili ya mwaka huu kwa kuzingatia vipimo vya ajira vya shirka la taifa la takwimu (KNBS).
Hata wale ambao wangali kazini wamepunguziwa saa za kazi kutoka saa 50 hadi 38 kwa wiki.
Kulingana na ripoti hiyo, moja kati ya biashara za kifamilia zimekwama kwa wakati huu na mbaya zaidi ni kuwa kati ya Februari na Juni, mapato ya biashara za kifamilia yalipungua kwa takriban asilimia 50.
“Hali hii ilizidishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha ambao uliongezea watu uchungu na mateso,” inaeleza ripoti hiyo.
Karibu kampuni zote zilishuhudia mauzo yakipungua kwa asilimia 50. Ripoti inasema kwamba asilimia 93 ya kampuni zote ziliripoti kupungua kwa mauzo katika muda wa siku 30 zilizopita ikilinganishwa na kipindi sawa mwaka wa 2019.
Ni asilimia mbili ya kampuni zilizoripoti kuimarika kwa mauzo na kwamba moja katika kampuni tano nchini Kenya ilipunguza idadi ya wafanyakazi.
Kufuatia hali hii, benki ya dunia imechunguza matarajio ya uchumi wa Kenya na kusema utadorora kwa asilimia moja 2020 au asilimia 1.5 hali ikiwa mbaya zaidi.
“Hatua hii imechukuliwa kwa kuzingatia hali mbaya iliyoshuhudiwa Aprili 2020, kuzingatia kwamba athari za janga hili zimekuwa mbaya zaidi kufikia sasa kuliko ilivyotarajiwa ukiwemo mchango wa sekta ya elimu kufuatia kufungwa kwa shule Machi,” ripoti inaeleza.
Hali hii ya kusikitisha inafichua kwa nini serikali ya Kenya ina presha kujadili upya milima ya madeni yake na inaomba muda zaidi wa kulipa madeni ya kimataifa ili iweze kukabiliana na athari za janga la corona.