BBI: Uhuru, Raila wapuuza vilio
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga jana Jumatano walipuuza wito wa makundi mbalimbali kuwa pawepo mashauriano kuhusu ripoti ya Muafaka wa Maridhiano (BBI) kwanza kabla ya kuzindua mchakato wa ukusanyaji saini za kuidhinisha kura ya maamuzi.
Wawili hao walizindua ukusanyaji saini za wapigakura wanaounga mkono mswada wa marekebisho ya katiba, licha ya wito wa wengi kuwa pawepo fursa ya ziada ya kushauriana kuhusu vipengee kadhaa kwenye ripoti hiyo.
Vilevile, uzinduzi huo ulipuuza wito wa wananchi wengine wanaosema kuwa wakati huu kuna matatizo mengi kama vile janga la corona lililoathiri uchumi sana, ambayo yanafaa kutatuliwa badala ya kuelekeza mawazo kwa marekebisho ya katiba.
Mswada unaopendekeza marekebisho ya katiba kupitia kwa BBI, umebainisha kuwa raia huenda wakabebeshwa mzigo mzito licha ya hali ngumu ambayo tayari inawakumba.
Katika muda wote tangu ripoti ya kwanza ya BBI ilipotolewa, kulikuwa na wito kutoka kwa viongozi mbalimbali, mashirika na raia wa kawaida waliotaka baadhi ya masuala yarekebishwe kwa manufaa ya umma.
Hata hivyo, mswada uliozinduliwa jana umeonyesha kuwa marekebisho yaliyofanyiwa ripoti hiyo yanalenga zaidi kutuliza nafsi za wanasiasa ambao watategemewa kufanikisha refarenda.
Mbali na nyadhifa mpya za uongozi kama vile waziri mkuu, manaibu wake wawili na cheo cha kiongozi rasmi wa upinzani, mswada huo umeongeza idadi ya maeneobunge kutoka 290 hadi 360.
Hii ina maana kuwa Bunge la Kitaifa litakuwa na jumla ya wabunge 366, pamoja na wabunge sita ambao watateuliwa kuwakilisha makundi ya watu wenye mapungufu ya kimwili na vijana.
Katika bunge la Seneti, mswada huo unapendekeza kwamba kila kaunti iwakilishwe na maseneta wawili, mwanamume na mwanamke. Hiyo ina maana kuwa idadi ya maseneta itapanda kutoka 67 hadi 94.
Aidha, hii ina maana kuwa Wakenya watahitajika kugharimia mishahara na marupurupu ya wawakilishi hawa wakati huu ambapo uchumi wa Kenya umeathirika pakubwa na janga la Covid-19.
Japo mswada huo unapendekeza kuwa nusu ya mawaziri watatoka bungeni, umependekeza kubuniwa kwa nyadhifa za manaibu wa mawaziri. Vyeo hivyo vipya sasa vitatambuliwa kikatiba endapo Wakenya wataidhinisha marekebisho hayo ya Katiba katika kura ya maamuzi.
Kilio kingine ambacho baadhi ya wananchi walikuwa wametoa, ni kuhusu pendekezo la kubuniwa kwa Baraza la Polisi Nchini (KPC).
Baraza hilo lingesimamiwa na waziri wa Masuala ya Ndani, hatua ambayo wadau wengi waliona kuwa sawa na kuingilia uhuru wa Idara ya Polisi hasa majukumu yanayosimamiwa na Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi (NPSC).
Ingawa mswada uliozinduliwa Jumatano uliondoa sehemu ya kubuni baraza hilo, kuna pendekezo kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi awe na mamlaka zaidi katika NPSC ambayo ni tume huru.
“NPSC ibadilishwe ili itambue mamlaka ya Inspekta Mkuu kama mwamrishaji mkuu wa idara ya polisi,” inasema sehemu ya mswada.
Vilevile, pendekezo tata kuhusu uteuzi wa afisi ya kupokea malalamishi kuhusu maafisa wa mahakama umepigwa msasa, ingawa bado unampa rais mamlaka ya kuteua atakayesimamia afisi hiyo.
Kulingana na mswada huu mshikilizi wa wadhifa huo sasa atateuliwa na rais kisha kuidhinishwa na Seneti.
Suala hilo liliibua pingamizi kali kutoka kwa baadhi ya viongozi wakiwemo wabunge na mawakili wakidai kuwa uteuzi wa mshikilizi wa afisi hiyo na rais utaingilia uhuru wa Idara ya Mahakama.
Mbali na hayo, sekta ya afya inayokumbwa na misukosuko mingi imeonekana kusahaulika katika mpango wa kurekebisha katiba.
Wadau katika sekta hiyo wamekuwa wakitaka kubuniwa kwa Tume ya Kitaifa ya Afya kusimamia masuala ya wahudumu wa afya, lakini hilo halijatajwa kwenye mswada wa BBI.
Miongoni mwa watakaovuna zaidi endapo mapendekezo hayo yatapitishwa ni madiwani ambao watatengewa hazina ya fedha za maendeleo. Madiwani pia wataruhusiwa kuwa mawaziri wa kaunti.
Vilevile, maseneta watapewa mamlaka ya kufanya maamuzi kadhaa ya kisheria bila kupitia Bunge la Taifa.
Kwa upande mwingine, magavana watapata afueni kuhusu bajeti kwani imependekezwa iwe kikatiba kwamba wapewe asilimia 50 ya bajeti endapo madiwani watakataa kupitisha mswada wa bajeti katika kaunti.
Kaunti 28 zimependekezwa kuongezwa maeneobunge ambapo Nairobi itapata 12, Nakuru (5), Kiambu (6), Kilifi (4), Mombasa (3) na zilizosalia kupata kati ya eneobunge moja hadi matatu.