• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Kiswahili: Wabunge waache visingizio

TAHARIRI: Kiswahili: Wabunge waache visingizio

KITENGO CHA UHARIRI

WABUNGE Novemba 26 waliingia Alhamisi ya tatu rasmi waliohitajika kuzungumza Kiswahili ndani ya Bunge la Kitaifa.

Sawa na Alhamisi mbili zilizopita, kulikuwa na vioja kwani wengine wao walitatizika sana kuzungumza lugha hiyo ya taifa.

Huwa ni aibu tunaposikia baadhi ya wabunge wakijitetea kuwa hawana uwezo kuzungumza Kiswahili kwa vile si lugha wanayoifahamu vyema.

Hawa ni wabunge wale wale ambao wakati wa kampeni unapofika, utawakuta wakiongea kwa ufasaha sana wanapoomba kura kwa wananchi.

Wanavyozungumza Kiswahili bungeni ni tofauti sana na jinsi wanavyoongea wanapotaka kura za wananchi mashinani ambao huwa ni vigumu kuelewa Kiingereza wanachokithamini hawa wabunge.

Badala ya kutoa vijisababu visivyo na msingi kuhusu kwa nini wanakumbwa na changamoto kuzungumza Kiswahili, ni vyema wajitahidi hadi wakati watakapokuwa na uwezo kikamilifu.

Wabunge na viongozi wengine wakuu wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kupeperusha bendera ya taifa hili kwa nchi za nje ambapo wao huzuru mara kwa mara.

Hii ni kumaanisha kuwa, wanafaa wawe na ufahamu kwa mapana kuhusu tamaduni za nchi hii, kuu kati yao ikiwa ni lugha ya Kiswahili.

Wale kati yetu ambao wamewahi kupata nafasi ya kutembelea nchi za nje, au hata kujumuika na raia wa kigeni wanaotembelea nchini humu wanafahamu sana jinsi raia hao hutaka kufahamu mengi kuhusu nchi yetu, ikiwemo kujifunza Kiswahili kutoka kwetu.

Hivyo basi, ni aibu ikiwa kiongozi anayeshikilia nafasi ya hadhi kubwa kama vile mbunge ataanza kushikwa na kigugumizi wakati mzungu anapotaka amwongeleshe Kiswahili.

Tunafahamu kuwa huenda mfumo wa elimu ambapo watoto mashambani hadi leo hufunzwa kwa lugha ya mama huenda uliathiri uwezo wa wengi kuzungumza vyama lugha ya taifa.

Hata hivyo, kungali kuna nafasi ya viongozi kujirekebisha na hata kujitwika jukumu la kuwa mabalozi wa Kiswahili katika maeneobunge wanayoongoza. Baada ya bunge la taifa kuaza kukumbatia Kiswahili, ni matumaini yetu kwamba hatua hii itaenezwa hadi katika mabunge ya kaunti ambapo madiwani katika baadhi ya kaunti husisitiza kuzungumza lugha zao asili bungeni.

You can share this post!

Rekodi ya Gor Mahia katika CAF Champions League kabla ya...

DAISY: Tuzae watoto tunaoweza kumudu mahitaji yao ya...