• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 6:55 PM
Liverpool wadandia kilele cha jedwali la EPL kwa kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Brighton

Liverpool wadandia kilele cha jedwali la EPL kwa kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Brighton

Na MASHIRIKA

PENALTI ya utata iliyofungwa na Pascal Gross mwishoni mwa kipindi cha pili iliwawezesha Brighton kusajili sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza mnamo Novemba 28, 2020 uwanjani American Express.

Penalti hiyo ilikuwa ya pili kwa Brighton kupokezwa katika mchuano huo baada ya fowadi Neal Maupay kupoteza mkwaju wa kwanza katika kipindi cha kwanza.

Liverpool ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL walidhani walikuwa wamechukua uongozi wa mapema kupitia kwa Mohamed Salah baada ya kushirikiana vilivyo na Roberto Firmino katika dakika ya 17. Hata hivyo, bao lake halikuhesabiwa na refa Stuart Attwell baada ya teknolojia ya VAR kuthibitisha kwamba lilifumwa wavuni akiwa ameotea.

Sajili mpya Diogo Jota alicheka na nyavu za Brighton katika dakika ya 60. Bao hilo lilikuwa lake la tisa hadi kufikia sasa tangu aingie katika sajili rasmi ya Liverpool mwanzoni mwa muhula huu.

Fowadi Sadio Mane aliingia uwanjani katika kipindi cha pili na akashuhudia bao lake pia likikataa kuhesabiwa baada ya kubainika kwamba alikuwa ameotea.

Liverpool waliondoka uwanjani Amex wakiwa wengi wa majuto baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi. Kusuasua kwao kuliwapa wenyeji motisha ya kuwavamia zaidi na Brighton wakapata fursa ya kusawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia penalti baada ya Andy Robertson kumchezea visivyo Danny Welbeck ndani ya kijisanduku.

Kocha Jurgen Klopp alionekana mwingi wa hasira akiondoka uwanjani huku akiwachemkia marefa waliosimamia mchuano huo kwa kutoa baadhi ya maamuzi ambayo kwa mujibu wake, yalipendelea Brighton.

“Tulinyima ushindi wa wazi na mabao bayana ambayo hata kipofu angejua ni ya halali. Ni hujuma na maonevu kwa Liverpool ambao kwa kweli walicheza vizuri, kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kuwazidi wenyeji wao katika kila idara. Haileti raha yoyote iwapo hali itazidi kuwa hivi,” akasema mkufunzi huyo raia wa Ujerumani.

Pigo zaidi kwa Liverpool ni jeraha ambalo kiungo James Milner. Brighton walilazimika kuondoa Maupay na Adam Lallana baada ya dakika nane pekee kutokana na majeraha.

Klopp alilalamikia pia maamuzi ya vinara wa EPL kuratibu mchuano wao dhidi ya Brighton kusakatwa mapema Novemba 28 ikizingatiwa kwamba walikuwa wamechuana na Atalanta ya Italia kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 25, 2020 ugani Anfield. Liverpool walipokezwa kichapo cha 2-0 katika mchuano huo.

Ushindi wa Liverpool uliwakweza kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 21, moja pekee mbele ya Tottenham Hotspur ambao watakuwa wageni wa Chelsea mnamo Novemba 29 ugani Stamford Bridge. Brighton kwa upande wao walipaa hadi nafasi ya 16 kwa alama 10.

You can share this post!

Obiri atamalaki mbio za nyika mjini Machakos

Leopards, Bandari na Kakamega Homeboyz waanza vyema kampeni...