• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 4:50 PM
Lewandowski asaidia Bayern kuwazima Stuttgart kwenye Bundesliga

Lewandowski asaidia Bayern kuwazima Stuttgart kwenye Bundesliga

Na MASHIRIKA

BAYERN Munich walidumisha pengo la alama mbili kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) baada ya kocha Hansi Flick kuongoza masogora wake kutoka nyuma na kupepeta Stuttgart 3-1 mnamo Novemba 28, 2020.

Lassana Coulibaly aliwaweka Stuttgart kifua mbele baada ya kushirikiana vilivyo na Silas Wamangituka katika dakika ya 20.

Hata hivyo, Kingsley Coman alisawazishia Bayern katika dakika ya 38 kabla ya Robert Lewandowski kufunga la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza. Douglas Costa wa Juventus anayechezea Bayern kwa mkopo alizamisha kabisa chombo cha Stuttgart mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kufungia kikosi cha Flick bao la tatu.

Bayern kwa sasa wanajivunia alama mbili zaidi kuliko RB Leipzig waliosajili ushindi wa 2-1 dhidi ya limbukeni Arminia Bielefeld. Ni pengo la alama nne ndilo linalowatenganisha Bayern na Borussia Dortmund waliopokezwa kichapo cha 2-1 na Cologne.

Philipp Forster nusura afungie Stuttgart bao la pili mwishoni mwa kipindi cha pili japo ushirikiano wake na Coulibaly ukashindwa kumzidi ujanja kipa Manuel Neuer.

Bao la Lewandowski lilikuwa lake la 12 kutokana na mechi nane za hadi kufikia sasa za Bundesliga na la 17 kutokana na mechi 18 zilizopita katika ngazi ya klabu na timu ya taifa mnamo 2020-21.

Mnamo Novemba 25, 2020, Lewandowski ambaye ni raia wa Poland alifunga bao lake la 71 katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na kufikia rekodi ya fowadi wa zamani wa Real Madrid, Raul Gonzalez ambaye ni wa tatu nyuma ya Lionel Messi na Cristiano Ronaldo katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote kwenye UEFA.

Bao la Lewandowski katika mchuano huo liliwasaidia kupepeta Red Bull Salzburg ya Austria 3-1 na kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA zikisalia mechi mbili zaidi za makundi.

Bao lililofungwa na Costa lilichangiwa na sajili mpya wa Bayern, Leroy Sane aliyesajiliwa mwishoni mwa msimu wa 2019-20 kutoka Manchester City ya Uingereza.

Bayern kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Atletico Madrid ya Uhispania kwenye gozi la UEFA mnamo Disemba 1, 2020 jijini Madrid kabla ya kuwaalika washindani wao wakuu ligini, Leipzig mnamo Disemba 5, 2020.

You can share this post!

BBI: Ruto atapatapa

BBI: Gavana Nyoro aongoza wakazi wa Kiambu kutia saini