• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 12:46 PM
Mashirika ya kijamii yaonya wanasiasa dhidi ya kuingilia utendakazi wa polisi

Mashirika ya kijamii yaonya wanasiasa dhidi ya kuingilia utendakazi wa polisi

Na CHARLES WASONGA

MASHIRIKA ya kijamii yamewasuta wanasiasa kwa kuingilia utendakazi wa polisi ilhali ni wao wamekuwa wakiendesha kampeni ya kulinda uhuru wa idara hiyo.

Chini ya mwavuli wa Kundi la Mashirika ya Kijamii (CSRG), mashirika hayo Jumapili yalisema haikuwa sawa kwa wanasiasa hao, akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, kukosoa kazi ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusiana na kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

“Wiki jana wanasiasa hawakustahili kuhoji jaribio la Mkurugenzi wa DCI George Kinoti kuchunguza upya kesi za ghasia zilizotokea miaka ya 2007 na 2008. DCI iko huru kuchunguza kesi zozote za uhalifu endapo itapata taarifa mpya za ujasusi; na kazi hii haipaswi kuingiliwa na wanasiasa,” akasema Mshirikishi wa Kitaifa wa CSRG Suba Churchill, kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Kulingana na Bw Churchil, kwamba wahasiriwa wa ghasia hizo waliofika katika makao makuu ya DCI Nairobi walidhani kwamba waliitwa kulipwa fidia, ni ishara tosha kwamba hawajatendewa haki miaka 13 baada ya kutokea kwa ghasia hizo.

“Hii ina maana kuwa Rais Uhuru Kenyatta na wanasiasa wenzake wanafaa kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ambayo ilipendekeza ridhaa kwa wahasiriwa – zikiwemo familia za wahanga – wa dhuluma za kihistoria kuanzia 1963 hadi 2008,” akaongeza.

Mnamo Jumatatu wiki jana jumla ya waathiriwa 150 wa ghasia hizo kutoka eneo la Rift Valley walifika katika makao makuu ya DCI, Nairobi kuandikisha taarifa mpya kufuatia kile kilichodaiwa kama vitisho vipya dhidi yao.

Akiwahutubia baadaye, Bw Kinoti alisema kuwa DCI itachunguza vitisho hivyo na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote “endapo tutapata ushahidi”.

“Kazi yetu kama polisi ni kuzima uwezekano wowote wa kutokea kwa uhalifu. Kwa hivyo, ningependa kuwahakikishia kuwa tutachunguza visa hivyo kwa njia huru na haki kwa lengo la kuwakamata wahusika. Wakati huu hatutafanya kazi ya kuokota maiti baada ya watu kuuawa kwa sababu za kisiasa,” akasema Bw Kinoti.

Akashifiwa vikali

Dakika chache baadaye wanasiasa wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto walimkashifu Kinoti kwa kufufua kesi za ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 eneo la Rift Valley kwa lengo la kumzuia (Dkt Ruto) kuwania urais.

“Najua kuwa lengo la Kinoti na wakubwa wake waliomtuma ni kuchochea uhasama wa kikabila katika eneo la Rift Valley kufaidi watu wengine katika siasa za urithi wa urais 2022. Ningependa kuwaambia kwamba hilo halitawezekana,” akasema Dkt Ruto.

Wandani wake kutoka Rift Valley wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen nao walimtaka Rais Kenyatta kumdhibiti Bw Kinoti ili asilete machafuko tena eneo hilo.

“Ikiwa ghasia zitatokea tena Rift Valley atakayelaumiwa ni Rais Kenyatta. Kwa hivyo, tunamwomba kumkanya Kinoti kwani hatua ya kuamsha kesi hizo itavuruga amani ambayo imedumu eneo hilo kwa miaka mingi,” akasema Bw Murkomen katika majengo ya Bunge, Nairobi akiandamana na zaidi ya wabunge 40 wa mrengo wa ‘Tangatanga’.

Mnamo Jumatano, wakati wa uzinduzi wa sahihi za kuunga mkono marekebisho ya katiba kupitia mswada wa BBI, Rais Kenyatta alimkaripia vikali Bw Kinoti kwa kile alichotaja kama “kufukua makaburi ya waliofariki” kwa kuanzisha upya kesi “ambazo zilikamilishwa.”

You can share this post!

Mahrez afunga matatu na kusaidia Man-City kudhalilisha...

Alaves waduwaza Real Madrid katika gozi la La Liga