Michezo

Alaves waduwaza Real Madrid katika gozi la La Liga

November 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

EDEN Hazard alipata jeraha jingine katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) ulioshuhudia waajiri wake Real Madrid wakipokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Alaves mnamo Novemba 28, 2020 uwanjani Alfredo di Stefano.

Hazard aliyekuwa akichezea Real kwa mara ya nne tangu mwanzoni mwa msimu huu, aliondolewa uwanjani katika dakika ya 28 baada ya kupata jeraha la mguu.

Penalti iliyochanjwa na Lucas Perez katika dakika ya tano iliwaweka Alaves kifua mbele baada ya Jose Nacho Iglesias kunawa mpira uliopigwa na Victor Laguradia kuelekea langoni mwa Real.

Luis Joselu Mato alizamisha kabisa matumaini ya Real kurejea mchezoni baada ya kupachika wavuni bao la pili la Alaves katika dakika ya 49. Goli hilo lilitokana na masihara ya kipa Thibaut Courtois aliyeshindwa kuondoa mpira kwa wakati katika eneo la hatari.

Real walifutiwa machozi na fowadi raia wa Brazil, Carlos Casemiro.

Real wanaotiwa makali na kocha Zinedine Zidane sasa hawajasajili ushindi wowote kutokana na jumla ya michuano mitatu iliyopita. Matokeo hayo yanawasaza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 17, sita zaidi nyuma ya viongozi Real Sociedad.

Villarreal wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 19 japo wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko nambari mbili Atletico Madrid waliocharaza Valencia 1-0 na kufikia idadi ya pointi 23 zinazojivuniwa na Sociedad.

Hazard, 29, alijiunga na Real mnamo 2019 baada ya kuagana rasmi na Chelsea kwa zaidi ya Sh21 bilioni. Ingawa hivyo, fowadi huyo raia wa Ubelgiji amewajibishwa na mabingwa hao watetezi wa taji la La Liga mara 27 pekee licha ya kununuliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha.

Hazard alikosa michuano ya mwanzo wa kampeni za msimu huu kutokana na jeraha la misuli kwenye mguu wake wa kulia na akachezeshwa mara tatu pekee kabla ya kuugua Covid-19 mwanzoni mwa Novemba 2020.

Tangu apone Covid-19, Hazard alichezeshwa dhidi ya Villarreal katika gozi la La Liga mnamo Novemba 21 na akafunga penalti katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyowakutanisha na Inter Milan ya Italia mnamo Novemba 25, 2020. Aliwajibika ugani kwa muda wa dakika 65 na 78 kwenye michuano hiyo miwili mtawalia.

“Natarajia kwamba jeraha alilopata ni dogo na atarejea ugani hivi karibuni. Hata hivyo, tunasubiri tathmini ya daktari na itakuwa pigo kubwa iwapo atalazimika kusalia mkekani kwa kipindi kirefu,” akasema Zidane.

Real waliokuwa wenyeji wa mchuano dhidi ya Alaves, walianza gozi hilo la La Liga bila ya huduma za Karim Benzema, Dani Carvajal, Federico Valverde na nahodha Sergio Ramos.

Mechi tatu ambazo Real wamepoteza ndiyo idadi kubwa zaidi ya michuano ambayo imewashuhudia bila ushindi baada ya kushuka dimbani mara 10 tangu mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.

Miamba hao wa Uhispania sasa wanajiandaa kusafiri Ukraine mnamo Disemba 1, 2020 kuvaana na Shakhtar Donetsk katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Ushindi katika mechi hiyo utawakatia tiketi ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora.