Michezo

KICHAPO EMIRATES: Arteta ajiinamia chini kwa aibu

November 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta amesema kwamba hana hofu yoyote kwamba atatimuliwa na Arsenal licha ya kikosi hicho kuweka rekodi ya mwanzo mbaya zaidi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) tangu 1981.

Hii ni baada ya Arsenal kupepetwa na Wolves 2-1 mnamo Novemba 29, 2020 katika matokeo ambayo yalishuhudia vijana wa Arteta wakipoteza mchuano wa EPL kwa mara ya tatu mfululizo katika uwanja wao wa Emirates.

Licha ya kujizolea alama tatu muhimu, raha ya ushindi wa Wolves uliyeyushwa na jeraha baya la mapema alilolipata fowadi Raul Jimenez baada ya kugongana vichwa na beki David Luiz wa Arsenal.

Arsenal kwa sasa wanashikilia nafasi ya 14 kwa alama 13 sawa na Crystal Palace baada ya kupoteza mechi tano kati ya 10 iliyopita ligini. Arsenal waliweka rekodi hiyo duni mwaka mmoja tangu wamtimue kocha Unai Emery kwa sababu ya matokeo mabaya.

“Kufutwa kazi ni jambo nililolijua siku ya kwanza nilipoamua kujitosa katika ulingo wa ukufunzi. Nafahamu kwamba siku moja nitatimuliwa au nitaachia mwingine mikoba ya kikosi ninachokinoa kwa sasa,” akasema Arteta.

“Kupoteza kazi ni jambo ambalo najua litafanyika siku moja katika taaluma hii ya ukocha. Lakini nisingetaka linihofishe. Kubwa zaidi kayika malengo yangu kwa sasa ni kukijenga kikosi na kuchochea wanasoka wangu kufanya vyema katika kila mchuano,” akaongeza.

Pedro Neto aliwaweka Wolves uongozini baada ya kushirikiana vilivyo na Leandro Dendoncker Adama Traore aliyechangia pia goli la pili lilifumwa wavuni na Daniel Podence baada ya Gabriel Magalhaes kusawazishia Arsenal.

Arsenal walisalia butu katika mchuano huo huku fataki zilizoelekezwa langoni mwa Wolves kupitia kwa Willian Borges, Pierre-Emerick Aubameyang na Bukayo Saka zikidhibitiwa kirahisi na kipa Rui Patricio.

Ushindi wa Wolves uliwapaisha hadi nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 17 sawa na Southampton waliopigwa 3-2 na Manchester United uwanjani St Mary’s.

Chini ya kocha Nuno Espirito, Wolves kwa sasa wanajiandaa kuvaana na mabingwa watetezi Liverpool mnamo Disemba 6 ugani Anfield huku Arsenal wakitarajiwa kuwaendea viongozi wa jedwali Tottenham Hotspur siku hiyo hiyo ya Disemba 6, 2020.

Kabla ya hapo, masogora wa Arteta watakuwa wamechuana na Rapid Vienna ya Austria kwenye Europa League mnamo Disemba 3, 2020.