Kingi ahimiza mbinu za kisasa za biashara
ALEX AMANI na KALUME KAZUNGU
GAVANA wa Kilifi Amason Kingi amehimiza kiwanda cha kutengeneza sharubati ya maembe cha Malindi Natural Juice Processors, kukumbatia mbinu za kisasa kuimarisha soko la bidhaa hizo.
Akizungumza mjini Malindi katika hafla ya kukabidhi wakulima wa maembe kiwanda hicho, Bw King alisema mbinu zinazotumika kwa sasa ni duni na zimechangia ukosefu wa soko.
“Yafaa tubadilishe mbinu za biashara za kiwanda hiki. Tulivyofanya zamani, mbinu zile kwa sasa haziwezi kutusaidia sababu mazingira yamebadilika,” alisisitiza Bw Kingi.
Hata hivyo, aliwahakikishia wakulima hao wa maembe kwamba serikali yake itawaunga mkono ili kuhakikisha ndoto yao inatimia.
Aliwashauri wanakili mapendekezo yao kupitia kwa Waziri wa Kaunti wa Biashara na Viwanda ili matakwa yao yaangaziwe na serikali yake.
Katika Kaunti ya Lamu, wakulima wa pamba wanalilia ukosefu wa soko licha ya mavuno fufufu mwaka huu.
Wakizungumza na wanahabari mjini Mpeketoni, walililia serikali ya kaunti na ya kitaifa kuwatafutia soko.
Kupitia Mwenyekiti wa Muungano wa Wakulima wa Pamba Kaunti ya Lamu, Bw Jospeph Migwi, walisema ukosefu wa soko thabiti na uharibifu wa wadudu ndizo changamoto kubwa zinazowakabili.
“Kila mwaka tunapanda pamba. Tunasumbuka sababu ya wadudu waharibifu na baada ya mavuno tunajipata hatuna soko. Wakulima wengi wamevunjika moyo na kujiondoa katika kilimo hiki.
“Ni matumaini yangu kwamba serikali itatutafutia soko la pamoja ili tuuze zao letu kwa bei nzuri,” akaeleza Bw Migwi akiomba Wizara ya Kilimo nchini iingilie kati kuwaepusha na madalali wakora, ili wapate ari zaidi ya kuendeleza kilimo hicho.
Kiwanda cha pamba
Mary Wairimu alieleza wasiwasi wake kwamba madalali wengi zaidi watajitokeza msimu huu ambapo wamevuna pamba kwa wingi Lamu, na kuinunua kwa bei duni.
Bi Wairimu pia aliomba kaunti kuanzisha kiwanda cha pamba eneo hilo ili kuwawezesha wakulima kuuza zao lao moja kwa moja kwa wanunuzi.
“Najua huu ni wakati wa madalali kufurika vijijini mwetu kununua pamba kwa bei duni wakijua hatuna soko thabiti. Ninaamini shida zote zitatatulika endapo kaunti itatujengea kiwanda cha pamba eneo letu,” akaeleza Bi Wairimu.
Naye Bw Julius Mwangi anaitaka serikali kuwafadhili wakulima wa Lamu kwa mbegu za kisasa za pamba ambazo pia zinastahimili wadudu.
Kauli ya wakulima hao inajiri wakati ambapo serikali ya Kaunti ya Lamu tayari imefichua mpango wa kujenga kiwanda cha pamba, ambacho inakadiriwa kitagharimu Sh 100 milioni.
Pamba hukuzwa kwa wingi katika maeneo ya Mpeketoni, Baharini, Uziwa, Tewe, Hongwe, Wetemere, Hindi na Witu katika kaunti ndogo ya Lamu Magharibi.
Zao hilo pia hukuzwa eneo la Faz katika kaunti ndogo ya Lamu Mashariki.