• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
TAHARIRI: Wazazi wawajibikie uhuni wa watoto

TAHARIRI: Wazazi wawajibikie uhuni wa watoto

KITENGO CHA UHARIRI

WAZAZI ndio wa kulaumiwa kutokana na visa vinavyoongezeka vya watoto kupatikana wakishiriki burudani za ulevi, matumizi ya dawa za kulevya na disko nyakati za usiku katika maeneo mbalimbali nchini.

Mnamo Novemba 22, watoto 44 walinyakwa katika Mtaa wa Mountain View viungani mwa mji wa Nairobi wakishiriki ulevi na matumizi ya dawa nyingine za kulevya. Baadhi wanadaiwa walikuwa wakishiriki densi nusu uchi na kufanya mapenzi kiholela.

Hata hivyo hiki si kisa pekee, kwa kuwa vingine vimeripotiwa katika miji ya Kisumu na Mombasa. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba wengi walionyakwa kwenye sherehe hizi za burudani ni wanafunzi wa shule.

Wanafunzi wengi bado wapo nyumbani kutokana na janga la virusi vya corona hata baada ya serikali kuwaruhusu wale wa gredi ya nne, darasa la nane na kidato cha nne kurejea shuleni miezi miwili iliyopita.

Swali hata hivyo ni je, wazazi wa watoto hawa wanaonyakwa wako wapi wakati ambapo wadogo hao hutoka nyumbani na kushiriki burudani hizi za usiku, ambazo zinapuuza hata kafyu iliyowekwa na serikali?

Si siri kwamba wazazi wengi hujishughulisha sana na kutafuta njia ya kuwakimu wana wao na kusahau majukumu yao ya malezi. Mzazi ataruhusu vipi mwanawe ambaye hajafika umri wa miaka 18 kuenda disco, ilhali anafahamu kwamba kuna kafyu na pia shughuli kama hizo huwapotosha wadogo hao?

Hii ndiyo maana mzazi pia anafaa achukuliwe hatua kali za kisheria iwapo mwanawe atapatikana kwenye visa hivi vya burudani kwa sababu atakuwa amefeli katika majukumu yake ya malezi.

Disko hizi pia zimechangia mimba za mapema miongoni mwa watoto wa kike ambao pengine hawatarejea shuleni mnamo Januari wakisubiri kujifungua.

Pia mikusanyiko hii ya vijana wanaoburudika ni kiini cha kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Ikizingatiwa kuwa tumeanza mwezi wa Disemba ambao huwa ni wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya, huenda visa vya vingi zaidi vikaripotiwa vya matineja kushiriki disco hizi, ulevi usiokuwa wa mipaka pamoja na tabia nyinginezo zisizokuwa za kimaadili.

Tayari maafisa kutoka idara inayohusika na masuala ya watoto wamelalamikia suala hili pia vyombo vya usalama vinafaa kuwa ange ili watoto wetu wasipotoke kimaadili.

You can share this post!

Wandani wa Ruto wataka Kinoti afutwe kazi

Kwa nini tunapinga BBI