Wahudumu wa afya wamshutumu Joho
Na WINNIE ATIENO
WAFANYAKAZI wa afya wanaoendelea na mgomo wao wamemtaka Gavana wa Mombasa Hassan Joho kusitisha kampeni za kisiasa Kaunti ya Kwale na badala yake ajikite katika kusuluhisha matatizo ya afya yanayogubika kaunti hiyo.
Aidha walimshtumu Bw Joho kwa kupuuza swala la sekta ya afya huku akiwaacha wakazi wa Mombasa wakitaabika kufuatia ukosefu wa huduma za matibabu, lakini akiendelea na kampeni za siasa.
Bw Joho amekita kambi Kwale akimpigia debe mwaniaji wa ODM Bw Omar Boga anayewania kiti cha ubunge wa Msambweni kilichoachwa wazi baada ya kifo cha Suleiman Dori.
Mgomo wa wahudumu hao wa afya ukiwemo wauguzi, wahudumu (clinical officers) na wengineo unoingia wiki ya tatu hii leo umelemaza shughli za kukabiliana na janga la corona. Ni madaktari pekee ambao wanaendelea kupambana na virusi vya corona katika hospitali za umma kaunti hiyo.
“Sekta ya afya inaendelea kudorora huku Bw Joho akiendeleza kampeni za kisiasa hivyo tunamuomba badala ya kukimya kuhusu matatizo ya huduma za matibabu aje azungumze jambo la kutufaa maana afya ni muhimu kuliko siasa,” alisema katibu wa chama cha wahudumu wa afya tawi la Mombasa Bw Peter Maroko.
Kaunti hiyo ambayo ni ya pili nchini kwa maambukizi ya corona ina zaidi ya visa 6,900.
Wafanyakazi hao wakiongozwa na wakuu wa vyama vyao waliandamana nje ya hospitali ya Pwani, wakimshtumu Bw Joho kwa kulifumbia macho swala lao ikiwemo ukosefu wa marupurupu ya kukabiliana na janga la corona, bima ya afya na vifaa vya kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.
“Shughuli za matibabu zimekwama katika hospitali za umma Mombasa tangu tuanze mgomo wetu. Tuliamua kugoma baada ya mwajiri kukosa kutimiza matakwa yetu hususan kucheleweshwa kwa mishahara mara kwa mara na kutufanya tuwe watu wa kukopakopa,” alisema Bw Franklin Maghanga katibu mkuu wa chama cha maafisa wa kliniki (Kenya Union of Clinical officers).
Bw Maghanga alisema hawatorejea kazini hadi pale matakwa yao yatakapotimizwa.
Walisema juhudi zao za kusitisha mgomo huo zimeambulia patupu baada ya mwajiri kushindwa kutekeleza matakwa yao.
“Inasikitisha kwamba wahudumu wa afya Kaunti ya Mombasa wanajizatiti kutoa huduma za matibabu lakini wanapougua wanashindwa kutumia bima ya afya sababu kaunti inachelewa kulipa. Kaunti iwasiliane na NHIF ili tunapougua tunatibiwa; tuna wasiwasi maana wenzetu wawili waliaga dunia baada ya kuambukizwa virusi vya corona,” alisema Bw Maroko.
Alisema wamelemewa na maambukizi ya virusi vya corona.
Hata hivyo serikali ya kaunti imeapa kusuluhisha mgomo huo.
“Tunafanya kila juhudi kumaliza mgomo ili warejee kazini. Tunafanya mkutano nao tutafute suluhu,” alisema Bw Denis Lewa wa serikali ya kaunti.