• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uhalifu: Wanakijiji wageukia waganga

Uhalifu: Wanakijiji wageukia waganga

Na MWANGI MUIRURI

WAKAZI wa eneo la Ichagaki, Kaunti ya Murang’a wametishia kukodisha mganga wa kienyeji kuwasaidia kukabiliana na ongezeko la visa vya uhalifu katika eneo hilo.

Wanasema kuwa maafisa wa polisi wameshindwa kumaliza magenge ya wahalifu ambayo yanajumuisha vijana wasio na ajira.

Kulingana na wakazi, vijana waliokuwa wakijihusisha na biashara ya pombe sasa wameingilia uhalifu kufuatia msako mkali dhidi ya watengenezaji wa mvinyo haramu.

Magenge ya vijana hao ambao wanatumia dawa za kulevya, sasa wanahangaisha wakazi wa eneo hilo kwa kuvamia makazi yao na kuwaibia.

Mmoja wa wajumbe wa kamati ya muungano wa wakazi wa eneo hilo, James Waweru aliambia Taifa Leo kijijini Kianjiru-ini kwamba wanahofia maisha yao kufuatia kuongezeka kwa magenge ya wahalifu.

“Tunajaribu kujiinua kimapato kwa kuwekeza katika mifugo lakini magenge ya vijana yanatuvamia na kutwaa mifugo hiyo kwa nguvu mchana,” akasema Bw Waweru.

Wanakijiji wanadai kuwa vijana hao wameiba kuku 200, mbuzi 10, nguruwe 18, ngombe wawili na punda mmoja.

Bw Waweru anasema maafisa wa polisi hawajakamata wahalifu hao licha ya wanakijiji kuripoti kituoni.

“Polisi wanatwambia kuwa tuweke bidii tukamate wezi hao wakiwa na ushahidi mkononi,” akasema.

“Kwa sababu imekuwa vigumu kuwakamata, tumeamua kutumia waganga wa mitishamba ili wawanase kwa kutumia mazingaombwe yao ili tusiendelee kupoteza mali yetu,” akaongezea.

Wanakijiji wanasema kuwa waganga hao wa mitishamba watawasaidia kunasa wahalifu hao.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa makanisa wamepinga hatua ya wanakijiji hao kukimbia kwa mganga wa mitishamba badala ya kuelekeza masaibu yanayowakumba kwa kanisani kwa njia ya kuomba Mungu.

Askofu Julius Kagiri wa kanisa la Holy Tabernacle Church of Christ anasema kuwa: “Ni aibu kwa wanakijiji ambao wengi wao ni Wakristo kuamini nguvu za giza kuwatatulia matatizo yao.”

Mnamo 2014, aliyekuwa Jaji Mkuu alitania kwa kusema kuwa kesi ndogondogo zinasababisha msongamano kortini na kuwahimiza Wakenya kutumia njia mbadala kutafuta suluhisho, ikiwemo kutumia waganga wa mitishamba.

Diwani wa eneo hilo, Charles Mwangi, alisema kuwa haungi mkono mpango huo wa kutumia waganga kutatua changamoto ya uhalifu katika eneo hilo.

Mbunge wa Maragua Mary wa Maua alimtaka waziri wa Usalama Fred Matiang’i kuongeza idadi ya maafisa wa polisi ambao watakuwa wakifanya doria kote kijijini humo.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Upandikizaji figo bado changamoto kwa...

Kocha Joachim Loew aponea shoka katika timu ya taifa ya...