• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 7:55 AM
Wanafunzi 78 wahepa shule ili kutahiriwa

Wanafunzi 78 wahepa shule ili kutahiriwa

Na FLORAH KOECH

ZAIDI ya wanafunzi 78 wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kisanana, Kaunti Ndogo ya Mogotio, Baringo, Jumanne walitoroka shuleni mwao katika hali ya kutatanisha.

Baadhi ya ripoti zilidai walifanya hivyo ili kushiriki kwenye shughuli ya upashaji tohara, inayoendelea eneo hilo.

Iliripotiwa wanafunzi hao waliondoka shuleni saa saba Jumanne usiku, huku wanafunzi 23 pekee wakibaki.

Mkurugenzi wa Elimu katika eneo hilo, Bw Robert Nyaberi, alisema bado hawajabaini sababu halisi ya wanafunzi hao kutoroka shuleni, ingawa wanatuhumu walitaka kushiriki kwenye shughuli hiyo ya kitamaduni ambayo inaendelea kwa sasa.

“Nilipokea ripoti kuwa zaidi ya wanafunzi 78 wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Kisanana walitoroka kutoka shuleni mwao nyakati za usiku, ambapo ni wanafunzi 23 pekee walibaki. Bado hatujabaini chanzo cha kitendo hicho. Hata hivyo, nimemwagiza mwalimu mkuu wa shule hiyo, kujaribu kuchunguza kiini cha kitendo hicho kutoka kwa wanafunzi waliobaki,” akasema Bw Nyaberi.

“Vile vile, nimetoa maagizo kwa shule kuandaa kikao cha kamati ya bodi inayosimamia nidhamu kuamua hatua itakayochukuliwa dhidi ya wanafunzi hao,” akaongeza.

Alisema wanashirikiana na wazazi wa wanafunzi husika kuhakikisha wamerejea shuleni ikizingatiwa wanatarajiwa kufanya mtihani kuanzia Ijumaa.

“Wanafunzi hao wanapaswa kurejea shuleni kwa kuwa wanatarajiwa kuanza mitihani yao Ijumaa. Nimewatuma maafisa wa elimu katika shule husika kufanya uchunguzi kamili kuhusu kilichofanyika, kwani tunataka ukweli kamili kuhusu tukio hilo. Ninatuhumu wengi walitaka kushiriki kwenye shughuli za upashaji tohara,” akasema.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, wanafunzi hao hawakuonyesha dalili zozote kwamba walikuwa wakipanga kutoroka kutoka taasisi hiyo kwani hawakusababisha uharibifu wowote.

Tukio hilo linajiri wiki tatu tu baada ya wanafunzi zaidi ya 46 kutoka Shule ya Upili ya Mseto ya Kiptoim kutoroka shuleni mwao, kwa kisingizio cha kuhofia kuambukizwa virusi vya corona. Kufuatia tukio hilo, ni wanafunzi wanne pekee walioachwa.

Ripoti zilieleza walifanya hivyo ili kushiriki kwenye shughuli ya upashaji tohara.

Hata hivyo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw Hezron Wainaina alisema tayari, wanafunzi 42 kati ya 46 waliotoroka washarejelea masomo yao.

You can share this post!

Watermelon mpya?

Aliyekaa jela miaka 14 aondolewa hukumu ya kifo