Habari Mseto

Aliyekaa jela miaka 14 aondolewa hukumu ya kifo

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BRIAN OCHARO

MWANAMUME aliyehukumiwa kifo kwa kosa la wizi wa mabavu amepata afueni baada ya hukumu hiyo kufutiliwa mbali.

Bw Kahindi Mwatsuma aliyekuwa akitumikia hukumu ya kifo sasa atakuwa huru huku akifanya kazi za kijamii kwa miaka mitatu.

Hii ni baada ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Malindi, Reuben Nyakundi kumpa kifungo cha nje na kuamrisha atolewe gerezani ampako amekaa kwa miaka 14.

“Mshukiwa ametumikia kifungo cha karibu miaka 14 kwa kosa hili. Kwa sababu hizi, ninaruhusu ombi lake na kubadilisha hukumu ya kifo. Mshukiwa atatumikia kifungo cha miaka 17 kwa sharti kwamba, kipindi kilichosalia cha miaka mitatu kiwe cha kuhudumia jamii chini ya usimamizi wa afisa wa kurekebisha tabia,” akaamua jaji.

Bw Mwatsuma ambaye amejaribu mara mbili bila mafanikio kubadilisha hukumu mbili za kifo kwa njia ya kukata rufaa atakuwa na bahati ya kutoka gerezani, ambapo amekaa tangu alipokamatwa mnamo 2006 kwakosa hilo.Majaribio mawili ya awali ya mshitakiwa, ambaye alikuwa mfanyabiashara wa mboga na samaki huko Kilifi kupata uhuru yalichochea Mahakama ya Rufaa kusitisha adhabu moja ya kifo aliyokuwa amepewa wakati wa hukumu ikimwacha kutumikia nyingine tangu alipopatikana na hatia ya wizi wa mabavu.

Baada ya hatua hizi kufeli, Bw Mwatsuma aliwasilisha ombi la kikatiba mbele ya Mahakama Kuu ya Malindi ambapo alipinga hukumu hiyo na kuiomba korti imwachilie huru.

Mshtakiwa huyo alidai mbele ya Jaji huyo kwamba, alikerwa na hakuridhika na hukumu ya kifungo kwa kosa hilo na kuongeza kuwa kufuatia kushtakiwa na hukumu ambayo pia ilithibitishwa na Mahakama ya Rufaa, hakuna shaka miaka 14 aliyotumikia kizuizini imemsaidia ipasavyo kubadilisha maisha yake.