Atletico Madrid bado pembamba Kundi A licha ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Bayern Munich kwenye UEFA
Na MASHIRIKA
ATLETICO Madrid sasa wana ulazima wa kuzuia kichapo dhidi ya RB Salzburg katika mchuano wao wa mwisho wa Kundi A ili kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.
Hii ni baada ya miamba hao wa Uhispania kulazimishiwa sare ya 1-1 na mabingwa watetezi Bayern Munich kwenye mojawapo ya mechi za Kundi A zilizosakatwa Disemba 1, 2020.
Bao la chipukizi Joao Felix katika dakika ya 26 lilikuwa limewatosha Atletico kusonga mbele kabla ya kiungo Thomas Muller kutokea benchi na kusawazishia Bayern kupitia penalti ya dakika ya 86 baada ya nyota huyo kuchezewa vibaya na Felipe.
Bayern tayari wamefuzu kwa hatua ya mwondoano ya UEFA japo rekodi iliyowashuhudia wakisajili ushindi katika jumla ya mechi 15 mfululizo za kipute hicho cha bara Ulaya sasa imekomeshwa.
Kocha Hansi Flick aliteua kupumzisha nyota wake wa haiba dhidi ya Atletico kwa minajili ya mchuano wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) utakaowakutanisha na RB Leipzig ambao kwa sasa wanasoma mgongo wao kwa karibu sana ligini.
Kati ya wanasoka walioachwa nje na Flick ni kipa Manuel Neuer, kiungo Leon Goretzka na fowadi Robert Lewandowski ambao hawakuwa sehemu ya kikosi kilichosafiri Uhispania. Serge Gnabry na Muller walipangwa kwenye kikosi cha akiba kabla ya kutokea benchi kwa minajili ya dakika 30 za mwisho.
Hatua hiyo iliwapa Bayern fursa ya kuwajibisha chipukizi wao wengi, wakiwemo Bright Arrey-Mbi na Jamal Musiala walioridhisha pakubwa dhidi ya Atletico ambao chini ya mkufunzi Diego Simeone, walijivunia maarifa ya wanasoka wao wote wa kikosi cha kwanza.
Musiala, 18, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kufungia Bayern mnamo Septemba 2020 alipokuwa sehemu ya wachezaji waliotikisa nyavu za Schalke katika ushindi wa 8-0 ligini.
Sare iliyosajiliwa na Atletico dhidi ya Bayern ilikuwa pigo kubwa kwa masogora wa kocha Simeone ambaye alishuhudia kikosi chake kilielekezea wageni wao makombora 13 huku Bayern wakilenga shabaha mara sita pekee.
Mbali na Marcos Llorente, mchezaji mwingine aliyeridhisha zaidi kwa upande wa Atletico ni chipukizi Joao, 21, ambaye anainukia vyema zaidi tangu asajiliwe kwa kima cha Sh15 bilioni kutoka Benfica ya Ureno mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.
Bao alilolifunga dhidi ya Bayern lilikuwa lake la nane msimu huu na la tatu kwenye kivumbi cha UEFA hadi kufikia sasa.
Joao atasalia kuwa tegemeo kubwa la Atletico katika mechi ya kufa-kupona itakayowakutanisha sasa na Salzburg ugenini mnamo Disemba 9, 2020. Salzburg watapania pia kutumia mechi hiyo kuendeleza rekodi nzuri iliyowashuhudia wakiwapepeta Lokomotiv Moscow 3-1 mnamo Disemba 1, 2020.