Habari Mseto

MKU yapata wahitimu wengi wa somo la sheria – ripoti

December 2nd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu Cha Mount Kenya (MKU) kilipata wanafunzi wengi kwenye mpango wa kuwatuma katika kazi za sheria.

Katika ripoti ya kutoka afisi ya sheria mwaka wa 2019-20 na jaji mkuu David Maraga, wanafunzi wapatao 837 walifuzu kwa somo la sheria.

Kulingana na ripoti hiyo, wanafunzi hao walitoka katika vyuo tofauti kama MKU, Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki, Africa Nazarene, Kabarak, Riara, na Chuo Kikuu Cha Kilimo na Sayansi cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

Orodha hiyo ya wanafunzi inaonyesha kuwa MKU iliongoza ikiwa na wanafunzi wengi waliofuzu wakiwa 215, UoN ilikuwa ya pili na wanafunzi 207, Kabarak 153, Riara 111, Chuo Kikuu Cha Kanisa Katoliki 79, Africa Nazarene 39, halafu JKUAT 33.

Kulingana na mpangilio uliopo kati ya mwaka wa 2019, Julai hadi Disemba 2019 MKU ilikuwa na wanafunzi 130 waliopata pahala pa kuendesha kazi zao. Halafu wengine 85 walipata nafasi mwezi Januari na Juni 2020.

“Tumepata heshima kubwa kwa wanafunzi wetu kupata nafasi ya kuingia katika idara ya sheria katika kitengo cha Parklands Jijini Nairobi. Pia tunashukuru idara ya sheria kwa kuwaoa mwongozo na maelekezo wanafunzi wa MKU hadi wakaongoza vyuo vingine,” alisema mkurugenzi katika chuo hicho Nelly Wamaitha.

Tayari wanafunzi waliofuzu wametumwa katika vituo tofauti katika idara ya sheria ili watekeleze wajibu wao.

Tangu MKU ilipozindua idara ya sheria imepiga hatua kubwa kwa sababu wengi wa wanafunzi waliohitimu wamepata ajira sehemu tofauti za nchi.

Wanafunzi wapatao 1,507 tayari wamefanikiwa kuingizwa katika idara ya sheria jambo linalowapa wengine motisha kujiunga na masomo ya sheria.