Michezo

Olunga afunga tena na kunusia taji la Mfungaji Bora katika Ligi Kuu ya Japan

December 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI matata wa Harambee Stars, Michael Olunga alifunga bao na kuchangia jingine katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na waajiri wake Kashiwa Reysol dhidi ya Vegalta Sendai katika Ligi Kuu ya Japan (J1-League) mnamo Disemba 1, 2020.

Olunga kwa sasa yuko pua na mdomo kutazwa Mfungaji Bora wa Msimu katika kampeni za Ligi Kuu ya Japan inayotarajiwa kutamatika rasmi mnamo Disemba 19, 2020 baada ya kupigwa kwa mechi sita zaidi muhula huu wa 2020-21.

Cristiano da Silva aliwafungulia Reysol ukurasa wa mabao katika dakika ya 21 kabla ya Olunga ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia kufunga la pili kunako dakika ya 60. Bao hilo la Olunga lilikuwa lake la 26 akivalia jezi za Reysol hadi kufikia sasa msimu huu.

Ilikuwa mara ya tatu kwa Olunga kufunga bao kambini mwa Reysol tangu kurejelewa kwa kivumbi cha J1-League kilichositishwa kwa muda mwishoni mwa Oktoba 2020 baada ya visa sita vya maambukizi ya Covid-19 kuripotiwa katika kambi ya waajiri wa Olunga.

Awali, Olunga ambaye kwa sasa anaselelea kileleni mwa wafunga bora katika kipute cha J1-League, alikuwa amefungia Reysol katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Sagan Tosu mnamo Novemba 21 na akacheka na nyavu kwa mara nyingine katika ushindi wa 4-1 uliosajiliwa na Kashima Antlers dhidi yao mnamo Novemba 25, 2020.

Katika mahojiano ya hivi majuzi na wanahabari nchini Japan, Olunga alisisitiza kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kufunga katika kila mojawapo ya mechi sita zijazo na kujipa uhakika wa kutawazwa Mfungaji Bora wa Mwaka.

“Nashukuru wachezaji wenzangu kwa kunipa fursa za kufunga mabao. Nitajitahidi zaidi katika michuano ijayo ili nifunge zaidi na hatimaye malengo yangu binafsi na ya kikosi kizima yatimizike,” akasema Olunga kwa kuonya kuwa kibarua kilichopo mbele yake si chepesi ikizingatiwa ukubwa wa presha anayokabiliana nayo.

Olunga alikosa kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Comoros katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2022. Stars waliambulia sare ya 1-1 jijini Nairobi katika mkondo wa kwanza kabla ya kupepetwa 2-1 katika mechi ya marudiano jijini Moroni.

Reysol wameratibiwa kuchuana na Nagoya Grampus katika mchuano wao ujao mnamo Disemba 5, 2020.

Chini ya kocha Nelson Baptista, Reysol watashuka ugani baadaye kuchuana na nambari 11 Oita Trinita (Disemba 9), nambari tano Cerezo Osaka (Disemba 12), nambari saba Sanfrecce Hiroshima (Disemba 16) kabla ya kuvaana na mabingwa wa msimu huu, Kawasaki Frontale mnamo Disemba 19. Reysol watafunga rasmi kampeni zao za msimu huu kwa kupepetana na FC Tokyo kwenye kivumbi cha kuwania taji la Levain Cup mnamo Januari 4, 2021.

Kawasaki Frontale tayari wametawazwa wafalme wa kivumbi cha J1-League msimu huu baada ya kujizolea jumla ya alama 75, 17 zaidi kuliko Gamba Osaka wanaoshikilia nafasi ya pili huku wakisalia na mechi nne zaidi za kusakata muhula huu.