• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Karata ya Naibu Rais kusukuma refarenda 2022

Karata ya Naibu Rais kusukuma refarenda 2022

Na WANDERI KAMAU

LENGO kuu la Naibu Rais William Ruto kuhusu pingamizi lake dhidi ya marekebisho ya katiba lilifichuka Jumatano, baada ya kukutana na viongozi wanaoegemea upande wake.

Akihutubia wanahabari nyumbani kwake Karen, Nairobi, Dkt Ruto alifichua kwamba angependa kura ya maamuzi ifanyike pamoja na Uchaguzi Mkuu ifikapo mwaka wa 2022.

Wadadisi wa kisiasa na baadhi ya viongozi wanasema, hili ni dhihirisho kuwa hatua yake kuitisha marekebisho zaidi ya mswada wa kurekebisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ni kwa lengo la kuchelewesha mchakato mzima.

“Najua watu wengi wanataka tuchukue msimamo, lakini mahali tulipo sasa yahitaji mashauriano kwa mapana. Naamini kuwa bado kuna nafasi kwetu kujadiliana na kuimarisha ripoti hiyo zaidi kwa kuzijumuisha kauli za watu na makundi ambayo yameeleza kutotosheka na mapendekezo yaliyojumuishwa,” akasema.

Dkt Ruto vile vile alisema kuwa kura ya maamuzi ikifanywa, Wakenya wasipige kura ya ndio au la bali kuwe na kila pendekezo litengwe ili wananchi waamue wanayotaka na kukataa yale wasiyoyataka katika mswada uliotolewa majuzi.

Hata hivyo, kauli yake ilikosolewa vikali na kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, aliyesema kuwa Dkt Ruto anaipotezea nchi muda.

“Uwepo wa maridhiano ni pendekezo zuri, lakini lazima tusipoteze muda. Lazima tufuate ratiba ya utekelezaji wa BBI kama ilivyo,” akasema.

Wadadisi walitaja mienendo ya Dkt Ruto kama njama ya kujisawiri kama kiongozi anayewajali Wakenya kabla 2022, kwani mirengo ya wanaoipigia debe ripoti hiyo na wale wanaoipinga i wazi.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga ndio wanaoongoza mrengo unaoiunga mkono ripoti huku Gavana Kivutha Kibwana (Makueni), kiongozi wa Narc-Kenya Martha Karua, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga kati ya wengine wakiwa miongoni mwa wale ambao wamejitokeza wazi kuipinga.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’, Prof Macharia Munene, ambaye ni mdadisi wa siasa, alisema lengo la Dkt Ruto ni kukataa kuwekwa kwenye kapu la wanaoipinga ripoti.

“Mkakati wa Dkt Ruto ni kujitokeza kama kiongozi anayewakilisha matakwa ya Wakenya, hasa baada ya kuorodhesha masuala ambayo bado makundi kadhaa yameeleza kutoridhishwa nayo. Yeye ni mwanasiasa, na ikizingatiwa ametangaza kuwania urais 2022, anajua taswira hiyo itampa uungwaji mkono miongoni mwa Wakenya wengi,” akasema Prof Munene.

Alisema kuwa kwa kuendelea kutoonekana kuipinga ama kuiunga mkono ripoti, Dkt Ruto anajenga taswira ya kiongozi ambaye hapingi maandalizi ya referenda na ambaye pia hawaachi wananchi kwenye masuala waliyotaja kutoridhishwa nayo.

Bw Javas Bigambo, ambaye pia ni mdadisi, alisema kwa kuchukua mwelekeo huo, Dkt Ruto anajua huenda ikawa rahisi kwa Wakenya kukataa baadhi ya mapendekezo ambayo yanaungwa mkono na kambi ya Bw Odinga.

“Anajenga jukwaa la kukabiliana na Raila 2022,”akasema.

Miongoni mwa mapendekezo ambayo Dkt Ruto na wandani wake walitoa jana ni kutathminiwa upya kwa mchakato wa kuteuliwa kwa Msimamizi wa Malalamishi katika Idara ya Mahakama.

Alisema msimamizi huyo anapaswa kuteuliwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) ama Jaji Mkuu, kinyume na pendekezo la sasa, ambapo anapaswa kuteuliwa na Rais na kupigwa msasa na Seneti.

Dkt Ruto pia alikosoa idadi ya wabunge, ambayo itaongezeka hadi 640. Badala yake, alipendekeza wawakilishi wa wanawake kuchaguliwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Alitaka pia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupewa mamlaka ya kuamua maeneo yanayohitaji kuongezwa maeneobunge, ili kuepusha ubaguzi wa maeneo yanayohitaji uwakilishi zaidi kama vile maeneo kame na yaliyotengwa kimaendeleo.

You can share this post!

BBI: Sahihi za kimabavu

Uingereza sasa yaidhinisha matumizi chanjo ya corona