• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
TAHARIRI: Machifu hawafai kuendesha BBI

TAHARIRI: Machifu hawafai kuendesha BBI

KITENGO CHA UHARIRI

MALALAMISHI kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba wanalazimishwa kutia sahihi kuonyesha wanaunga mkono kura ya maamuzi, yanatia doa mchakato mzima wa urekebishaji katiba.

Haikustahili kamwe serikali kuagiza maafisa wa utawala kama vile machifu na makamishna kuhusika katika shughuli ya ukusanyaji sahihi za BBI. Wengi wa maafisa hao wamejitetea kwamba hawalazimishi raia, lakini tusidanganyane, ziara kutoka boma moja hadi nyingine ambazo imethibitishwa zinafanywa na machifu maeneo kadhaa, zinatosha kushurutisha mwanakijiji kutia sahihi hata kama haungi mkono kura ya maamuzi.

Hii si mara ya kwanza kura ya maamuzi kuandaliwa nchini, na wanasiasa walikuwa na uwezo wa kuzungusha vijitabu vya kukusanya sahihi bila kuhusisha maafisa wa utawala katika shughuli hiyo.

Mchakato wa kurekebisha katiba ambao ulianzishwa kufuatia handisheki ya Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, umekuwa ukivumishwa kuwa na lengo la kuleta uwiano na utangamano kitaifa.

Inasikitisha kuwa, tangu mwanzoni mwa handisheki hadi sasa, matukio mengi yameshuhudiwa ambayo yanaibua maswali kuhusu kama kweli handisheki na Mpango wa Maridhiano (BBI) zitafanikiwa kutimiza malengo tunayoambiwa yanalengwa.

Katika hatua za mwanzoni kwa takriban miaka miwili iliyopita, tulishuhudia jinsi viongozi waliokuwa na msimamo unaotofautiana na ule wa BBI walivyokuwa wakiandamwa na kuadhibiwa.

Baadhi yao waliadhibiwa katika vyama vya Jubilee na ODM, wakapokonywa nafasi katika kamati za Bunge la Taifa na Seneti ikiaminika ni kwa vile walipinga matakwa na waasisi wa BBI.

Hivi sasa, malalamishi kutoka kwa wananchi kwamba wanatishiwa kunyimwa huduma muhimu endapo watakataa kutia sahihi kwa mswada wa kurekebisha katiba, yanaashiria mwendelezo wa utumiaji kifua kukamilisha safari iliyoanza wakati wa handisheki.

Mwelekeo huu si mzuri, na halisaidii kivyovyote ila kutoa nafasi ya wengi kuamini kuna nia fiche katika mpango mzima wa kurekebisha katiba. Demokrasia inayoongoza nchi hii inahitaji kuwa, kila mwananchi angepewa uhuru wa kujiambulia kama anataka marekebisho ya katiba au la.

Hata bila kutumia nguvu ya kushurutisha watu kutia sahihi, si siri kwamba viongozi wanaounga mkono marekebisho hayo bado hawangetatizika sana kufanikiwa kufikisha sahihi milioni moja ambazo zinahitajika na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuendeleza mbele mpango wa kuandaa kura ya maamuzi.

You can share this post!

Nzige wavamia mashamba na malisho Lamu

Nahodha wa Harambee Starlets atua kambini mwa Thika Queens...