Sonko ajua hajui

COLLINS OMULO na FADHILI FREDRICK

NJAMA, vitimbi na vioja vya Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko kujaribu kujinasua kutoka kwa ‘kinywa cha mamba’ katika bunge la kaunti hiyo, Alhamisi ziligonga mwamba madiwani walipopiga kura kwa wingi ili atimuliwe mamlakani.

Madiwani 88 wa Kaunti ya Nairobi walipiga kura kupitisha hoja ya kumtimua mamlakani gavana huyo, huku waliopinga hoja hiyo wakiwa ni madiwani wawili pekee.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa, kuna uwezekano wa uchaguzi mdogo wa ugavana Nairobi endapo Seneti itaidhinisha uamuzi wa bunge la kaunti.

Hii ni kutokana na kuwa kaunti hiyo haina naibu gavana ambaye anaweza kuchukua usukani endapo Bw Sonko atafurushwa.

Jaribio la kwanza la madiwani kumtimua Bw Sonko liligonga mwamba mnamo Februari Rais Uhuru Kenyatta alipoingilia kati.

Wakati huo, wadadisi walisema Rais alikuwa anaepusha hali ambapo kungehitajika uchaguzi mdogo, na pia kuzuia kukwamisha shughuli za kaunti sababu hakuna naibu.

Katika jaribio hili la pili ambalo lilianzishwa wiki kadhaa zilizopita, gavana huyo aliweka juhudi tele ikiwemo kuwaficha baadhi ya madiwani na kuwasafirisha nje ya Nairobi ili wasishiriki katika kikao cha kujadili hoja ya kumtimua.

Vituko hivyo Alhamisi viliendelea kuzingira shughuli nzima ya kupitisha hoja hiyo.

Mbali na matukio yaliyozingira madiwani, Jaji James Rika aliyekuwa akisikiliza kesi ambapo Bw Sonko alipinga kung’olewa mamlakani, alijiondoa katika kesi hiyo ghafla na hivyo kulemaza matumaini ya gavana huyo kuokolewa kortini.

Pande zote mbili za madiwani, wanaomuunga mkono gavana huyo na wanaompiga, walijihusisha katika vituko na vioja wakitaka kutimiza malengo yao.

Kwa upande mmoja, madiwani wanaomuunga mkono Bw Sonko walijitahidi sana kumwokoa kwa kuzuia hoja ya kumng’oa isipite katika bunge la Kaunti, huku wanaompinga wakijizatiti kupitisha hoja hiyo.

Mnamo Jumatano, madiwani wanaoegemea upande wa Bw Sonko walisafiri hadi Kwale ambako waliendelea kukaa hadi Alhamisi.

Ilisemekana kuwa njama yao ilikuwa kuzuia kuwepo kwa idadi ya kutosha ya madiwani kuendeleza hoja ya kumtimua Gavana.

Hata hivyo, ilipofika Alhamisi mchana, Kiongozi wa Wachache katika bunge la Kaunti, Bw Michael Ogada, aliruhusiwa kuisoma hoja hiyo mbele ya madiwani 58 waliokuwepo bungeni.

Katika sheria za bunge, palihitajika kuwepo na madiwani 42 ndani ya bunge au wanaohudhuria vikao kwa njia ya video.

Kwa jumla, bunge hilo lina madiwani 122 lakini 12 walifukuzwa katika vyama vyao kwa muda, na hivyo kubakisha madiwani 110 waliokubaliwa kupiga kura.

Madiwani waliofukuzwa na vyama vyao kwa muda ni wanachama wa Jubilee na ODM.

Imesemekana viongozi wa vyama hivyo, Rais Uhuru Kenyatta na Bw Raila Odinga mtawalia, walikuwa wamekubali gavana huyo atimuliwe.

Awali, Bw Sonko na wandani wake walikuwa wamejigamba kuwa wana idadi kubwa ya madiwani kwa hivyo walikuwa na hakika ya kumwokoa. Hata hivyo, mambo yalienda mrama wakati madiwani waliohudhuria kikao walipohesabiwa, na hatimaye kupiga kura.

Polisi walidumisha usalama mkali nje ya bunge la kaunti hiyo tangu asubuhi kwani ilihofiwa pangekuwa na purukushani.

Katika Kaunti ya Kwale ambapo madiwani wanaounga mkono Bw Sonko walikongamana maskani yake ya Kimerimeta, walikusanyika na kubeba mabango yaliyoandikwa nambari ili kudhihirisha kuwa walikuwa wengi. Ilibainika walikuwa takriban madiwani 57 pekee wala si zaidi ya 80 walivyokuwa wakidai awali.

Wote walihitajika kusalimisha simu zao za rununu, yamkini kwa nia ya kuwazuia wasishawishiwe kubadili msimamo wao na kuhudhuria vikao kwa njia ya mtandaoni.

Lakini wakati hesabu ya madiwani waliokuwa bungeni kibinafsi au kupitia kwa mtandao ilipoanza kuchukuliwa, baadhi ya waliokuwa Kwale walieleza mshangao kuwa waliorodheshwa kuwa wanahudhuria kikao hicho ilhali hawakuwa wameingia katika mtandao wa vikao vya bunge la Kaunti.

Takriban madiwani 20 kati ya 57 wanaoegemea upande wa Bw Sonko walidai akaunti zao za kuhudhuria vikao vya bunge kwa njia ya mtandao zilifunguliwa bila wao kujua.

Diwani wa Waithaka, Bw Anthony Karanja alikashifu jinsi hoja ya kumng’oa Sonko ilivyokuwa inaendeshwa kwa kutumia akaunti za madiwani ambao walikataa kushiriki katika vikao hivyo vya bunge.

“Tunakashifu tukio hili ambalo linaturudisha nyuma na kuangamiza demokrasia. Kama hamtakomesha yale mambo mnayofanya Nairobi basi huu ni mwisho wa demokrasia,” akasema, akisisitiza hawatakubali matokeo.

Madiwani waliokuwa Kwale ni wanachama wa vyama tofauti ikiwemo Jubilee, ODM, Wiper miongoni mwa vyama vingine.

Bw Sonko amelaumiwa kwa masuala mbalimbali ikiwemokushindwa kutekeleza wajibu wake wa ugavana licha ya kupunguziwa majukumu baada ya kukabidhi mengine kwa serikali kuu.

Amekuwa akimshambulia wazi Rais Uhuru Kenyatta katika siku za hivi majuzi, huku akiendelea kukashifu Idara ya Huduma za Nairobi (NMS).

Habari zinazohusiana na hii

Maseneta roboti

Sonko azongwa

Sonko nje

Ni gavana spesheli?